Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Viwanda (UNIDO)
limesema litasaidia Watanzania kutimiza ndoto za kuwa taifa lenye uchumi wa
kati linalotegemea viwanda kwa kuunga mkono utendaji wa pamoja wa sekta ya umma
na binafsi.
Kauli hiyo imetolewa katika hafla ya
chakula cha mchana iliyoandaliwa na Sekta Binafsi kwa Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO
Li Yong ambaye alikuwa katika ziara ya kwanza nchini Tanzania na pia ya kwanza
nje ya makao makuu ya Shirika hilo baada ya kuchaguliwa kwake kwa mara ya pili
mwaka jana.
Alisema katika hotuba yake kwamba moja ya
majukumu makubwa ya shirika hilo ni kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu
(SDGs) hasa lengo namba tisa la maendeleo na teknolojia
kwa ajili ya ustawi wa nchi hizo.
Aidha alisema ili kufanikisha hilo
kumesisitizwa ushirikiano ambao ni lengo namba 17 la SDGs.
Alisema sekta binafsi ikishirikiana vyema
na serikali ndiyo inayoendesha uchumi hasa katika kutoa fursa za kazi kwani
asilimia 80 ya kazi kila mwaka hutolewa na sekta binafsi.
Alisema katika hotuba yake hiyo kwamba
amefurahishwa na malengo ya Tanzania na nia ya Shirika hilo kuona kwamba
malengo hayo kuelekea uchumi wa kati wa viwanda yanatekelezwa kwa kuangalia
vionjo muhimu.
Aidha alisema kwamba wataendelea
kushirikiana na sekta binafsi kupitia TSPF kuhakikisha kwamba wananchi
wanashirikishwa katika malengo ya maendeleo ili kuwa na malengo endelevu na
yanayozingatia mazingira.
Naye Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini-
TPSF Dr. Reginald Mengi akizungumza katika hafla hiyo aliitaka UNIDO kusaidia
kutengeneza utajiri nchini Tanzania.
Dr. Mengi alisema kwamba ziara ya kiongozi
huyo imekuja wakati muafaka, wakati ambapo Tanzania inaelekeza macho yake
katika uchumi wa kati na hivyo kuwa na nafasi ya kusaidia ndoto hiyo kufanikiwa.
Alisema wakati nchi nyingi zimekuwa
zikipiga maendeleo, zimekuwa na msingi dhaifu wa uchumi wa viwanda kutokana na
kusafirisha zaidi bidhaa ambazo hazijasindikwa au zinazotokana na uziduaji.
Alisema hali hiyo pamoja na kuipa utajiri
nchi imekuwa haitawanyi utajiri uliopo.
Alisema kutokana na hali hiyo, UNIDO ina
kazi kubwa ya kusaidia Tanzania kufikia lengo lake la viwanda hata kusaidia
kuanzishwa kwa maeneo ya viwanda (Industrial Park).
Aidha aliishukuru UNIDO kwa kuwezesha
sekta binafsi na serikali kukaa pamoja kupitia Baraza la Taifa la Biashara
ambako kunakuwa na mazungumzo yenye tija kuhusiana na maendeleo ya biashara na
uchumi nchini Tanzania.
Alifafanua kwamba UNIDO ina nafasi kubwa
ya kuisaidia Tanzania hasa katika mipango mikakati yake kwa kuunganisha sekta
binafsi na umma ili kuiharakisha Tanzania kuelekea uchumi wa kati wenye
kutegemea viwanda.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda pamoja na Kimataifa Dr Augustine
Mahiga, ambaye wizara yake ndiye ilimwalika Mkurugenzi mkuu huyo, pamoja na
kumshukuru kwa kuitikia wito huo aliitakabkusaidia kuchagiza maendeleo ya
viwanda.
Alisema kwamba viwanda vya Tanzania bado
vichanga na vinahitaji kusaidiwa na kupewa nguvu ya kuendelea mbele kwani
pamoja na uchanga wake mchango wake katika kuelekea uchumi wa kati ni mkubwa.
Awali kabla ya hafla ya chakula cha mchana
UNIDO ilitiliana saini na serikali ya Tanzania waraka wa kusaidia kuitoa
Tanzania katika mipango ya kitaifa kwenda kwenye mipango ya nchi na washirika
ili kufikia uchumi wa kati.
Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es
Salaam kati ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles
Mwijage pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, Li Yong huku yakishuhudiwa na
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
No comments:
Post a Comment