Naibu waziri wa nishati Mhe. Subira Mgalu amewaahidi umeme wa
uhakika wakazi wa mitaa mbalimbali kwenye kata nne zilizopo katika jimbo la
Ukonga mkoani Dar es Salaam.
Mhe. Mgalu ametoa ahadi hiyo
mapema siku ya jana Jumamosi Februari 24, 2018 alipofanya ziara katika jimbo
hilo ambapo alifanya mikutano Zaidi ya sita kwenye maeneo tofauti tofauti
ambayo hayana miundombinu ya umeme.
Maeneo ambayo Mhe. Mgalu
alitembelea ni pamoja na: mtaa wa Bombambili kwenye kata ya Kivule, mtaa
wa Mbondole, Luhanga na Kiboga kwenye kata ya Msongola, mtaa wa Zogowale
kwenye kata ya Zingiziwa, mtaa wa Yongwe na Virobo kwenye kata ya Chanika, na
kata ya Buyuni .
Wananchi wengi wakiongozwa na
mbunge wa jimbo hilo Mhe. Mwita Waitara (CHADEMA), madiwani na wenyeviti wa
mitaa mbalimbali, walijitokeza katika mikutano hiyo ambapo walimweleza Mhe.
Mgalu kilio chao cha kutokuwepo na umeme katika maeneo hayo pamoja na maeneo
yenye huduma za jamii mfano, shule za msingi na sekondari, zahanati, na visima
vya maji.
Aidha wananchi hao pia
walimweleza Mhe. Mgalu kuhusu kuwepo kwa matukio yanayohatarisha hali ya ulinzi
na usalama kutokana na maeneo hayo kutawaliwa na giza nyakati za usiku.
Katika kujibu hoja hizo za
wananchi pamoja na Mhe. mbunge Waitara, Mhe. Mgalu aliwaeleza kuwa
serikali ya awamu ya tano baada ya kuona changamoto ni kubwa maeneo hayo
imepanga kupeleka miundombinu ya umeme kupitia wakala wa umeme
vijijini REA chini ya mradi wa Peri Urban ambapo tenda ya mradi huu
imeshatangazwa na tathimin imeshafanyika na REA ipo katika hatua za
mwisho za kumpata mkandarasi wa kutekeleza mradi huo.
Katika mikutano hiyo Mhe.
Mgalu pia amekemea uwepo wa vishoka wanaochangisha wananchi fedha kwa ajili ya
kulipia nguzo jambo ambalo amesema ni kinyume kabisa na utaratibu unaotumika
katika kuwaunganishia umeme wananchi.
Aidha Mhe. Mgalu aliwaasa wananchi
kutorubuniwa na kikundi au mtu binafsi kwa ajili ya kuchangia mradi huo na
kwamba gharama ya kuunganisha umeme kupitia miradi ya REA ni Tshs. 27,000 tu na
si vinginevyo.
Kwa upande wake mbunge wa
jimbo hilo Mhe. Waitara akiongea kwa niaba ya wananchi ameishukuru serikali ya
awamu ya tano kwa kusikia kilio cha wananchi wa maeneo hayo na kubuni mradi
utakaowapelekea umeme katika maeneo yao.
Aidha Mhe. Waitara aliwataka
wananchi hao kutoa ushirikiano wa kutosha pindi mradi utakapoanza kutekelezwa
huku akiwaomba kushirikiana na vyombo vya usalama katika kuwabaini mafundi
vishoka ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Katika ziara yake hiyo Mhe.
naibu waziri aliambatana na wataalamu kutoka TANESCO mkoa wa Pwani, wilaya ya
Ilala na Kisarawe, REA, wizara ya nishati, na wanahabari.
No comments:
Post a Comment