Msichana mwenye umri wa miaka 25, Anastazia Elias, mkazi wa Kata
ya Kipindu wilayani Nkasi mkoani Rukwa, amenusurika kifo baada ya kuokolewa na
polisi akituhumiwa kumuua mtoto wake baada ya kujifungua.
Wananchi wakiwa na silaha za jadi yakiwemo mawe walianza
kumshambulia mwanamke huyo wakimtuhumu kumuua mwanawe wa kiume baada ya
kujifungua ambapo alimviringisha na vipande vya khanga na kumuweka kwenye
kikapu alichokificha chini ya uvungu wa kitanda chake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo lililotokea juzi saa nane mchana katika Kijiji cha
Kipundu kilichopo mjini Namanyere.
Kamanda Kyando amesema mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Polisi
wilaya Nkasi na kwamba atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa tukio
kukamilika. Wakizungumza baadhi ya wanawake wamedai mtoto huyo alizikwa
juzi usiku katika kaburi lililochimbwa ndani ya nyumba ambayo mama yake mzazi
anaishi na bibi yake.
No comments:
Post a Comment