Kukua kwa sayansi na teknolojia kumeleta WiFi inayowaruhusu watu wengi kutumia intaneti kutoka kwenye chanzo kimoja bila kuhitaji kuunganishwa na nyaya.
WiFi ni teknolojia ya mtandao inayotumia mawimbi ya redio kutoa huduma za intaneti yenye kasi kubwa. WiFi na simu za mkononi huongeza hatari ya ujauzito kuharibika mimba kwa asilimia 48, utafiti unaonyesha.
Miali ya usumaku ni mlolongo wa mawimbi ya nishati yanayosafiri kwa kasi ya mwanga inayotokana na mzunguko wa umeme wa usumaku mfano mawimbi ya redio (radio frequency), mionzi mikali ya jua (ultraviolet) au miali isiyoonekana (infrared).
Hapo zamani, watafiti wamewahi kugundua kuwa miali ya usumaku inayotolewa na minara ya simu na nyaya za umeme mkubwa husababisha msongo kwenye mwili unaoharibu chembe za urithi (jeni) tatizo linaloweza kusababisha kuharibika kwa mimba kwa wajawazito.
Miali ya usumaku ambayo kila mmoja wetu humpata kwa viwango tofauti, zamani ilihusishwa na ugonjwa wa saratani na Shirika la Afya Duniani lilipendekeza utafiti zaidi ufanyike kuona athari zake kwa wajawazito.
Watafiti wa kituo cha utafiti Kaiser kilichopo Oakland, Marekani waliwachunguza wajawazito 913 wenye mimba za umri tofauti na kugundua baadhi Wajawazito walikuwa washaharibikiwa angalau mara moja kwa vipindi vilivyopita.
Wajawazito wote walipimwa viwango vya mionzi kila siku na kifaa kijulikanacho kama Emdex Lite Meter. Watafiti walifuatilia matokeo ya kila mjamzito.
Utafiti
Watafiti waligundua wajawazito waliokuwa kwenye miali ya hali ya juu waliongeza hatari ya mimba kuharibika kwa asilimia 48 kuliko wale waliokuwa kwenye viwango vya chini.
Wajawazito waliokuwa kwenye viwango vikubwa vya miali, asilimia 24.2 waliharibikiwa mimba ikilinganishwa na asilimia 10.4 ya wale waliokuwa kwenye miali ya viwango vidogo.
Watafiti wanadai hatari hutokea bila kujali mwanamke aliwahi kuharibikiwa mimba au la. Kiongozi wa utafiti huo, Dk De-Kun Li alisema: “Utafiti huu unatoa ushahidi kwa watu kwamba miali ya usumaku huathiri afya ya binadamu kibaiolojia.”
Sababu nyingine
Nchi zilizoendelea kwenye masuala ya tiba kama Marekani wajawazito huharibika mimba kati ya asilimia 15 na 20. Nchi zinazoendelea kama Tanzania hakuna takwimu rasmi za mimba kuharibika ingawa tatizo linaweza kuwa kubwa kuliko nchi zilizoendelea.
Kitaalamu tunasema mimba imeharibika yenyewe ikiwa chini ya wiki 20 sawa na miezi mitano. Mara nyingi mimba huharibika miezi mitatu ya mwanzo ingawa mimba yaweza haribika miezi mitatu ya pili.
Mimba ikiharibika miezi mitatu ya mwanzo mara nyingi hutokana na kusababishwa na mtoto mtarajiwa. Inakadiriwa mimba nne zinazoharibika hutokea miezi mitatu ya mwanzo.
Wataalamu wanadai mimba ikiharibika miezi mitatu ya pili (kati ya wiki ya 14 na 26) basi inaweza kuwa imesababishwa na tatizo la kiafya alilonalo mjamzito. Vile vile mimba kuharibika baada ya wiki ya 26 huwa ni kwa sababu ya mfuko wa maji kupasuka kabla ya wakati kutokana na maambukizi kumzunguka mtoto. Na mara chache hutokea njia (shingo ya kizazi) inapofunguka kabla ya wakati.
Sababu za kuharibika mimba miezi mitatu ya mwanzo zinatia ndani matatizo ya kromosomu (nyuzi nyuzi katika kiini seli cha kila kiumbe ambazo hubeba viiniurithi yaani jeni), matatizo ya plasenta au kondo la nyuma.
Plasenta hupitisha lishe kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuondosha taka za kimetaboli za mtoto. Plasenta huanza kufanya kazi kuanzia mwezi wa tatu wa ujauzito.
Vitu vinavyoongeza hatari ya kuharibika mimba ni pamoja na umri. Mmoja kati ya wanawake 10 wa chini ya miaka 30 huharibikiwa mimba Kwa wanawake wenye miaka 35 hadi 39 wanawake wawili kati ya 10 huharibikiwa mimba na kwa wanawake walio na miaka zaidi ya 45, zaidi ya nusu ya mimba zote huharibika.
Vitu vingine vinavyoongeza hatari ni pamoja na unene, uvutaji sigara wakati wa ujauzito, matumizi mabaya ya dawa mfano Ibuprofen au Misoprostol, kunywa kafeini zaidi ya miligramu 200 kwa siku, unywaji wa vileo uliokithiri zaidi ya viwango viwili vya vileo kwa wiki.
Kiwango kimoja cha kileo ni sawa na bia (lager) moja, mililita 25 za pombe kali (spirits) glasi ya mililita 125 ya divai au mvinyo ni sawa na kiwango kimoja na nusu. Sababu za kuharibika mimba miezi mitatu ya pili hujumuisha matatizo ya kiafya ya muda mrefu mfano kisukari, kupanda sana kwa shinikizo la damu, ugonjwa wa figo na magonjwa ya tezishingo (thyroid). Maambukizi ya magonjwa kama vile surua, Ukimwi, kaswende, kisonono na malaria pia husababisha mimba kuharibika.
Nyingine zinazochangia mimba kuharibika ni kula chakula chenye sumu au vyakula visivyoiva vizuri mfano nyama na mayai mabichi. Sababu nyingine ni kizazi kuwa na umbo lisilo la kawaida, kulegea kwa shingo ya kizazi na ovari kuwa kubwa kuliko kawaida hali inayosababisha mabadiliko ya homoni.
Kupunguza athari za WiFi, simu
Kuweka simu mbali na tumbo pia kutohifadhi simu kwenye mifuko ya nguo zao husaidia kupunguza athari kufika tumboni na kusababisha madhara kwa mtoto.
Inashauriwa uzime WiFi ikiwa huitumii hasa wakati umelala. Kuweka simu kwenye hali ya ndege (airplane mode) ikiwa huitumii. Kutumia waya wa sauti (speakerphone) wakati ukiongea, vilevile inashauriwa kutozungumza kwa muda mrefu.
Hivyo ni vyema kuwa mchaguzi bora wa maneno. Kutotumia vifaa vinavyotoa miali ya usumaku mfano kifaa chochote kinachotumia umeme unapokuwa kwenye gari kwa maana viwango vya miali vinakuwa juu tayari.
Fikra potofu
Kuongeza hatari ya mimba kuharibika hakuhusiani na hali ya kihisia ya mjamzito mfano kuwa na msongo au huzuni, kuwa na mshtuko kutokana na jambo fulani, kunyanyua vitu vizito, kufanya mazoezi mzazito ya viungo ingawa inapendekezwa kuwasiliana na daktari ili akupangie aina ya mazoezi ya kufanya kulingana na hali yako.
Nyingine ni kufanya kazi wakati wa ujauzito mfano kukaa au kusimama muda mrefu, kufanya ngono kipindi cha ujauzito, kusafiri kwa anga (ndege) na kula vyakula vyenye viungo vingi.
Napenda kuwatia moyo walioharibikiwa mimba kutoogopa kutafuta mimba tena baada ya mimba ya mwanzo kuharibika.
Na Dk Joachim Mabula, Mwananchi
NINI MAONI YAKO
No comments:
Post a Comment