Siku moja baada ya Mwananchi kuripoti habari ya Alex Suke (18) anayedaiwa kupigwa risasi na polisi waliokuwa wakituliza vurugu eneo la Buguruni Relini Ijumaa iliyopita, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Temeke Dk Amani Malima, amethibitisha kumpokea kijana huyo.
Akizungumza jana na mwandishi wetu, Dk Malima alisema madaktari wanaendelea kumpatia matibabu na kubainisha kuwa juzi alishindwa kuthibitisha tukio hilo kwa maelezo kuwa hakuwepo ofisini, “Yupo wodi namba saba lakini kamuone Dk Mwita ambaye yuko zamu atakupa ushirikiano,”alisema.
Mwananchi lilipowasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula kwa njia ya simu alisema, “hilo suala ni la zamani sana wewe ndo unaulizia leo? Kwa sasa nipo nje ya ofisi nitakutafuta baadaye kidogo.”
Awali, mwandishi wetu alimtafuta Dk Mwita ambaye alikuwa zamu katika wodi namba saba alikolazwa kijana huyo.
Baada ya kufika wodini hapo saa saba mchana alishuhudia madaktari wakifanya maandalizi kwa ajili ya kumpeleka kijana huyo kwenye chumba cha upasuaji jambo lililozuia mahojiano wakati huo.
Mwandishi wetu aliweka kambi kwa muda hospitalini hapo kwa ajili ya kuzungumza na daktari huyo na kujibiwa na wasaidizi wake kuwa ana majukumu mengi, si rahisi kupata muda wa kuzungumza na mwanahabari.
Mama wa kijana huyo, Aghata Mwangamba alisema madaktari walimueleza kuwa mwanae atafanyiwa upasuaji wa mkono ambao ulijeruhiwa kwa risasi huku akilalamikia mzigo wa gharama za matibabu. “Leo (jana) analalamika sana mkono tofauti na jana (juzi) na madaktari wameniambia leo (jana) watamfanyia upasuaji mwingine wa mkono ambao ulijeruhiwa na risasi,” alisema.
Alisema wameiomba Serikali iwasaidie katika matibabu kwani hadi sasa ametumia Sh900,000 katika matibabu.
“Mtoto wangu hana bima na mimi ni mjane gharama ni kubwa na uwezo wangu kwa sasa umekuwa mdogo,” alisema mama huyo na kubainisha kuwa anategemea genge kuendesha maisha yake.
Bibi wa kijana huyo, Subira Mwakajila alisema familia imepata pigo kwa kujeruhiwa kijana huyo, “Sisi hatuoni haja ya kupelekana mahakamani lakini tunataka kujua hatma ya kijana wetu kiafya na kimasomo,”alisema.
Kijana huyo alipigwa risasi wakati polisi wakiwatawanya watu maeneo ya Buguruni Relini Ijumaa iliyopita.
Juzi baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo akiwamo Juma Liwanje walieleza kuwa kijana huyo alipigwa risasi kutokana na vurugu zilizotokea eneo la Buguruni Relini baada ya askari kufyatua risasi kuwatawanya watu wakiwamo madereva bodaboda.
Home »
» DAR ES SALAAM: Hospitali ya Temeke yathibitisha kumpokea kijana aliyejeruhiwa kwa risasi
No comments:
Post a Comment