MELI 19 ZA UVUVI ZATIWA KITANZINI NCHINI TANZANIA

Meli zipatazo 19 zimetozwa faini ya jumla ya shilingi bilioni 19 kutokana na  kubainika kufanya uvuvi haramu na uchafuzi wa mazingira katika ukanda wa uchumi wa bahari kuu.
Hayo yamesemwa na waziri wa mifugo na uvuvi, Luhaga Mpina siku ya jana Ijumaa Februari 23, 2018 jijini Dar es Salaam ambapo alisema  kuwa uamuzi huo umefuatia meli hizo kukiuka Sheria ya uvuvi wa bahari kuu kwa kutoripoti katika bandari za Dar es Salaam, Zanzibar, Mtwara au Tanga kwa ajili ya ukaguzi kabla ya kuondoka katika bahari kuu ya Tanzania.
Mpina amesema mbali na kutakiwa kulipa faini hizo, serikali pia imeiagiza Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) kuwaandikia notisi wamiliki wa meli hizo kutaarifu maamuzi hayo na kuijulisha kamisheni ya kusimamia samaki aina ya Jodari Bahari ya Hindi (IOTC) hatua zilizochukuliwa na serikali kwa meli hizo.
“Kwa kitendo hiki cha kukiuka masharti haya ya leseni zao maana yake wameshiriki uvuvi haramu, wamechafua mazingira” alisema Waziri Mpina.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), Hosea Mbilinyi alizitaja meli hizo zilizopigwa faini ambapo kila moja itapaswa kulipa faini ya shilingi bilioni moja kuwa ni pamoja na: Tai Hong no.2,  Tai Hong no. 8, Tai Xiang no.5, Tai Xiang no.5, Tai Xiang no. 8, Tai Xiang no. 9, Tai  Xiang no. 10, Tai Xiang no.7, Tai  Xiang no 6, Tai Hong no .7.
Mbilinyi ameongeza kwa kuzitaja meli zingine kuwa ni pamoja na: Xian Shiji no. 81, Xin Shiji no. 82, Xin Shiji no. 83, Xin Shiji no. 86, Xin Shiji no. 76, na Jian Shen no. 1.
Katika hatua nyingine Mpina alisema eneo la bahari kuu lenye ukubwa wa kilomita za mraba 223,000 limekuwa likinufaisha mataifa mengine na kwamba msimamo wa serikali kwa sasa ni kuhakikisha rasilimali zilizomo ndani ya eneo hilo zinachangia katika ukuaji wa pato la taifa.


Share:

No comments:

SIKILIZA JAMII FM

Blog Archive

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

HABARI KUU WIKI HII

WAENDESHA BLOG

Contact Form



Recent post