Wizara ya Nishati nchini imewataka watanzania kuchangamkia fursa
za mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki.
Hayo yalisemwa na naibu
waziri nishati Mhe. Subira Mgalu kwa niaba ya waziri wa nishati katika hotuba
yake ya kufunga kongamano la wadau kuhusu fursa za mradi wa bomba la mafuta
ghafi la Afrika Mashariki lililofanyika Jana Februari 23, 2018.
Katika kongamano hilo
lililoandaliwa na baraza la uwekezaji la taifa chini ya ofisi ya Waziri Mkuu na
Wizara ya Nishati ambalo lilifunguliwa na Waziri wa Nchi Sera, Bunge, Uratibu,
Ajira, Kazi na Vijana, Mhe. Jenister Mhagama (Mb).
Mada mbalimbali
ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na: taarifa fupi ya mradi,fursa zilizopo kwenye
mradi huu wa bomba la mafuta ghafi, sheria ya mafuta ya mwaka 2015 juu ya
vifungu vinavyohusiana na ushiriki wa watanzania, fursa zilizopo katika sekta
ya bima zinazopatikana na mradi huu, na umuhimu wa viwango na ithibati
zinazohitajika katika mradi huo.
Mada hizo zilitolewa na
Wizara ya Nishati, TOTAL, EWURA, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima TIRA, na TBS.
Katika kongamano hilo, Mhe.
naibu waziri aliwataka washiriki kutumia taarifa walizozipata kupitia mkutano
huo katika kujipanga zaidi na kuhimili ushindani wakati wa kutangaza kazi
mbalimbali kipindi cha ujenzi wa mradi huo na uendeshaji wake, na kutumia fursa
ya mazingira mazuri yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha Mhe. Mgalu amesema
serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli ina
nia ya dhati kabisa ya kuweka mazingira wezeshi katika miradi mikubwa hii
ili kuwawezesha Watanzania kufaidika na mradi huu wa bomba la mafuta ghafi.
Serikali za Tanzania na
Uganda zilisaini makubaliano ya Kutekeleza Mradi huu kupitia Tanzania 1 Machi
2016 na bomba hili litapita kwenye mikoa nane Kagera ,Geita , Shinyanga, Tabora
,Singida ,Dodoma ,Manyara na Tanga pamoja na Wilaya 24 na Kata 134.
Bomba hili litakuwa na urefu
wa jumla ya Kilometa 1443 kutoka Hoima Uganda hadi eneo la Chongoleani mkoani
Tanga kati ya hizo kilometa 1147 zitakuwa upande wa Tanzania .
Mhe naibu waziri amewapongeza
waandaji na wadhamini wa kongamano hilo na kuwashukuru washiriki zaidi ya mia
nne waliohudhuria na kuahidi wizara ya nishati itaendelea kuandaa mikutano
mbali mbali ya wadau kwa ajili ya kupeana taarifa za fursa na
kupanga mikakati ya namna ya ushiriki madhubuti wa watanzania katika nyanja
mbalimbali ikiwemo ajira za kitaalam na ajira za kawaida , huduma za kibima na
kibenki, huduma za vyakula , sekta ya ujenzi na usafirishaji, nakadhalika.
No comments:
Post a Comment