Ushirikiano
wa Kibiashara kati ya Tanzania na India umeendelea kuimarika kutokana na
kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa zinazouzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo
mbili. Hayo yalisemwa na Mheshimiwa Sandeep Arya, Balozi wa India nchini
Tanzania wakati wa Kongamano la Kukuza Biashara kati ya India na Mtwara
lililofanyika jana Jumamosi tarehe 3 Machi, 2018 katika Ukumbi wa NAF Hotel
Apartment, Mjini Mtwara.
Balozi Sandeep alisema asilimia
24 ya mauzo ya bidhaa za Tanzania nchi za nje kwa mwaka 2017 ziliuzwa nchini
India. Mwaka 2017 Tanzania iliuza nchini India bidhaa zenye thamani ya Dola za
Kimarekani 977.5 ambapo ilinunua bidhaa mbalimbali kutoka nchini India zenye
thamani ya Dola za Kimarekani 1,165.
Alisema mauzo ya bidhaa za Tanzania zilizouzwa India mwaka 2017
yaliongezeka kwa wastani wa asilimia 38 ikinganishwa na mauzo ya mwaka 2016.
Hii ilitokana na
ongezeko la bidhaa zilizozalishwa nchini ambazo zilihitajika kwa wingi huko
India zikiwemo dhahabu, korosho n.k. Aidha, Balozi huyo alisema ili kuimarisha
biashara kati ya Tanzania na India, Serikali ya India imeondoa tozo za ushuru
kwa baadhi ya bidhaa zinazosafirishwa kutoka Tanzania kwenda India zikiwemo
korosho, mchele n.k na pia imefuta gharama za kibali cha kuingia India (Visa)
kwa wafanyabiashara kutoka Tanzania na kubaki 7,000 tu.
Kongamano hilo liliandaliwa kwa ushirikiano baina ya Chama cha
Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mtwara na Ubalozi wa India
nchini Tanzania.
Karim Faida – JAMII FM.
No comments:
Post a Comment