Magonjwa ya figo yanakadiriwa kuwaathiri takribani wanawake milioni 195 duniani kote na yanashika nafasi ya 8 kama chanzo cha vifo vya wanawake duniani na inakadiriwa kuwa wanawake 600,000 hupoteza maisha kutokana na matatizo ya figo duniani kote kila mwaka
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile wakati akitoa tamko la siku ya Figo duniani ambapo huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi.
Dkt.Ndugulile alisema tafiti zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha wanawake wako katika hatari zaidi ya kupata matatizo ya figo ukilinganisha na wanaume. Kwa wastani asilimia 14% ya wanawake wanaathiriwa na matatizo ya figo ukilinganisha na asilimia 12% kwa wanaume
Kwa upande wa Tanzania Naibu Waziri huyo alisema ugonjwa huo umekuwa ukiongezeka na tafiti zilizofanya Kanda ya Kaskazini mwaka 2014, ulionyesha kuwa kati ya 7% – 15% ya Watanzania wana matatizo sugu ya figo na kwa asilimia kubwa yamekuwa yakichangiwa na magonjwa ya Shinikizo la Damu na Kisukari
Hata hivyo aliongeza kuwa kwa utafiti uliofanywa na Hospitali ya Kanda Bugando, umeonesha kuwa 83% ya Wagonjwa wa Kisukari wana matatizo sugu ya figo na kati ya hawa, 25% walikuwa wanahitaji huduma za usafishaji damu.
“Wagonjwa waliokuwa wanapatiwa huduma ya kusafisha damu kutokana na figo kushindwa kufanya kazi, ambao ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) walikuwa 178. Kwa sasa idadi ya Wagonjwa hawa imeongezeka na kufikia 783.
Aidha, alisema mgonjwa mmoja anahitaji wastani wa shilingi milioni 37 kwa mwaka kwa ajili ya kulipia gharama ya kusafisha damu. Aidha, anahitaji kusafiri na kufika kwenye huduma kwa wastani wa safari 126 kwa mwaka sawa na wastani wa safari 3 hadi 4 kwa wiki.
Alisema Serikali imekuwa ikipeleka wastani wa wagonjwa thelathini na tano(35) kwa mwaka nje ya nchi kwa ajili ya kupandikiza figo na idadi ya waliokwishapandikizwa figo na ambao wanafuatiliwa matibabu yao katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni takribani 204.“Gharama za kupandikiza figo nje ya nchi ni wastani wa fedha za Kitanzania milioni 75 hadi 77 kwa mtu mmoja,ikijumuisha upandikizaji,nauli na malazi”Alisema Dkt.Ndugulile
Dkt.Ndugulile alitoa wito kwa wananchi kubadili jinsi ya kuandaa vyakula nyumbani, mfano kwa kupunguza kiasi cha chumvi kwenye chakula na kiasi cha mafuta kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza magonjwa shinikizo la damu (hypertension), kisukari na unene wa kupindukia, vile vile kuhamasisha familia kufanya mazoezi.Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya figo ya mwaka huu wa 2018 ni “FIGO NA AFYA YA WANAWAKE: WASHIRIKISHWE, WATHAMINIWE NA WAWEZESHWE”.
CHANZO: AFYABLOH Na WAMJW. Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment