Waziri Mkuu Azindua Mpango Mkakati Wa Afya Moja



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mpango Mkakati wa Afya Moja na Dawati la Kuratibu Afya Moja nchini ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa mahala safi na salama kwa kuishi na kufanya kazi za kimaendeleo.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 13, 2018) wakati akizindua mpango mkakati huo katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, ambapo amesema dhana ya Afya Moja inafaa kutumika zaidi katika nchi zinazoendelea.

Waziri Mkuu amesema mbali na mpango kufaa kutumika katika nchi zinazoendelea pia hata kwa nchi zinazokaribia maeneo ya wanyama pori kama Tanzania kutokana na kukabiliwa na changamoto ya upungufu wa rasilimali.

Amesema kwa upande wa nchi za Afrika hali ni hatarishi zaidi kwa kuwa Bara hilo, lina sehemu nyingi zinazokaribia mapori makubwa ya wanyama kama Bonde la Mto Kongo, ambalo mazingira yake yamekuwa ni kitovu cha magonjwa ya mlipuko kama vile Ebola, Homa ya Bonde la Ufa (RVF), Marburg na mengineyo.

Waziri Mkuu amesema kwa kutambua hilo, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na wadau wengine wa Maendeleo, imeendelea kutekeleza agenda ya Afya Moja nchini tangu mwaka 2013 ilipozinduliwa kwa mara ya kwanza mjini Arusha na  Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Mohamed Gharib Bilal.

“Utekelezaji wa Mpango huu unakwenda sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2015-2020) ya kujenga Taifa lenye watu wenye afya bora itakayowawezesha kuzalisha mali na kutoa huduma mbalimbali ambayo ni muhimu sana katika kufikia azma ya Serikali ya kujenga Uchumi wa Viwanda.”

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama alisema uzinduzi wa mkakati huo ni ngao tosha kwa nchi katika kuzuia na kudhibiti magonjwa.

Alisema pamoja na kutekeleza kanuni za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ambazo zinahitaji ushirikiano  wa sekta mbalilmbali kwa kutumia dhana ya afya moja, mpango mkakati huo unaleta msukumo katika Ofisi ya Waziri Mkuu  kuendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali kudhibiti magonjwa.

Bibi Jenista alisema uratibu wa afya moja unakwenda sambamba na matakwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (IOE) na Shirika la Kimataifa la Chakula la Kilimo (FAO) ambayo yanashirikiana katika kudhibiti magonjwa yanayoambukiza na usugu wa dawa.
Share:

No comments:

SIKILIZA JAMII FM

Blog Archive

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

HABARI KUU WIKI HII

WAENDESHA BLOG

Contact Form



Recent post