Benki ya Dunia (WB) ofisi ya Tanzania imekanusha madai ya kwamba iliishinikiza Serikali kusimamisha zoezi la bomoa bomoa ya makazi ya watu kwenye hifadhi ya barabara ya Morogoro.
Madai hayo ambayo yaliripotiwa na chombo kimoja cha habari, kabla ya kusambaa kwenye mitandao ya jamii yalibainisha kwamba WB walishinikiza kusimamishwa kwa bomoabomoa kwa kuwa ndio wafadhili wa mradi wa barabara hiyo.
Ilidaiwa na vyombo hivyo kuwa WB ilitishia kusimamisha utoaji wa fedha kwa ajili ya upanuzi wa barabara hiyo, ambayo itakuwa na miundombinu ya barabara ya mwendokasi (BRT) pamoja na barabara kuu kuelekea Morogoro, mpaka hapo fidia itakapolipwa.
Akitolea ufafanuzi madai hayo leo Februari 13, 2018 msemaji wa ofisi ya WB Tanzania, Loy Nabeta amesema ofisi yake haijatoa taarifa yoyote ya kuitaka Wakala wa Barabara (Tanroads) kisitisha bomoa bomoa hiyo.
“Tunaelewa kwamba gazeti lilifanya mahojiano na baadhi ya wamiliki wa nyumba. Benki ya dunia inathamini sera na utaratibu unaotakiwa kufuatwa kutekeleza mradi wowote ule inaoufadhili,” amesema msemaji huyo.
“Hizi ni nyaraka za kisheria ambazo tulisaini na Serikali kwa kila mradi tunaoufadhili na huwa tunahakikisha kwamba utekelezaji wake unafuata utaratibu.”
Msemaji huyo aMEsema wamepokea malalamiko mengi mwaka jana kutoka kwa wamiliki wa nyumba zilizojengwa pembezoni mwa barabara ya Morogoro ambao walipewa notisi ya kubomoa na Tanroads.
“Tuliwawasilisha malalamiko serikalini. Desemba 22, 2017, tulipata barua toka kwa katibu mkuu wizara ya ujenzi, mawasiliano na uchukuzi kwamba watasimamisha ubomoaji wa nyumbakwenye kipande cha kuanzia Ubungo hadi Kimara,” amesema kwenye taarifa hiyo.
Amesema bomoa bomoa hiyo ambayo ilitekelezwa kuanzia Kimara hadi Kiluvya, ni mwendelezo wa utekelezaji wa upanuzi wa barabara ya Morogoro, haihusiani na mradi wowote unaofadhiliwa na WB.
Bomoa bomoa hiyo inahusisha nyumba na mejengo 1,300 ambavyo vinadaiwa kujengwa kwenye hifadhi ya barabara ambayo ni meta 121.5 toka katikati ya barabara ya sasa. Hata hivyo, nyumba 1,000 zimekwisha bomolewa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, upanuzi wa barabara ya Morogoro (kutoka Kimara hadi Kiluvya) unatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa.
CHANZO: MPEKUZI HURU
No comments:
Post a Comment