Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Zainab Telack amewataka wananchi
mkoani Shinyanga kutoa taarifa sahihi kwa watafiti wanaofanya Utafiti wa Mapato
na Matumizi ya Kaya Binafsi mkoani humo.
Telack ametoa rai hiyo leo Ijumaa Februari 23,2018 katika mkutano na
waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga akizungumzia Utafiti wa Mapato na
Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/2018.
Utafiti huo unaosimamiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) unaoendelea
nchini katika kata 796 utazifikia kaya 9,552 nchini ambapo kaya 408 zitafikiwa
katika kata 34 za mkoa wa Shinyanga.
Telack alisema njia pekee ya kufuatilia utekelezaji wa program za
maendeleo ni kufanya tafiti mbalimbali kama huu unaoendelea ambao unalenga
kutoa takwimu za hali ya umaskini na takwimu nyingine ili kuisaidia serikali na
wadau kutathmini hatua zilizofikiwa katika kutimiza malengo ya kitaifa.
“Suala la ukusanyaji wa takwimu rasmi za serikali ni shirikishi na ni
wajibu wa kila mwananchi kutoa taarifa sahihi,natoa wito kwa viongozi kuanzia
ngazi ya mitaa,vitongoji,vijiji,kata,wilaya na mkoa kutoa ushirikiano wa karibu
kwa watafiti watakaozifikia kaya 408 zilichaguliwa katika mkoa wetu”,alisema
Telack.
“Utafiti huu wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa mwaka
2017/2018 unahitaji sana ushirikiano kutoka kwa wananchi wote hasa katika kaya
zilizochaguliwa kitaalamu kuwakilisha sampuli za kaya zilizopo mkoani
Shinyanga”,aliongeza.
Alibainisha kuwa kila kaya iliyobahatika kuchaguliwa itahojiwa kwa siku
14 mfululizo na mdadisi atakutana na mkuu wa kaya ambaye hatatakiwa
kubadilishwa ili kupata takwimu sahihi kwa ajili kupanga maendeleo ya
nchi.
Mkuu huyo wa mkoa alisema utafiti huo utasaidia kuweka msingi katika
kutambua viashiria vya msingi vya kiuchumi,ajira na ustawi wa jamii ambavyo
vitatakiwa kufuatiliwa kwa kipindi husika na kupata makadirio ya jumla ya
mwenendo wa matumizi ya kaya ili kuandaa fahirisi za bei.
Telack alizitaja kata 34 za mkoa wa Shinyanga zitakazofanyiwa utafiti
kuwa ni Ngokolo,Mwawaza,Ndala,Ndembezi,Songwa,Mwadui
Lohumbo,Kishapu,Mwakipoya,Lagana,Talaga,Didia,Mwakitolyo,Iselamagazi,Mwamala,Nyida
na Lyabusalu.
Kata zingine zitakazofikiwa ni Lyamidati, Lunguya, Chela, ,Jana, Isaka,
Chambo, Igunda, Sabasabini, Bulungwa, Ushetu, Ubagwe, Mondo, Nyahanga, Zongomera,
Nyihogo,Majengo na Kilago.
Kwa upande wake Meneja wa Takwimu (NBS) wa mkoa wa Shinyanga,
Evarist Tairo alisema huo ni utafiti wa saba tangu nchi ipate Uhuru na utasaidia
kwa kiasi kikubwa kupata takwimu halisi za mapato na matumizi ya kaya binafsi.
No comments:
Post a Comment