DK. KIGWANGALLA AAGIZA MBINU MPYA ITUMIKE KUDHIBITI WANAOCHIMBA MADINI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS kujenga kituo cha ulinzi cha kudumu katika eneo la chanzo cha maji ya mto zigi kilichopo ndani ya Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani kwa ajili ya kulinda chanzo hicho.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari  baada ya kutembelea eneo la chanzo hicho na
kukuta uharibifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya wananchi wanaodaiwa kuchimba madini ya dhahabu katika eneo hilo la hifadhi kinyume cha sheria
“Nimeagiza
 watu wa TFS wajenge kituo cha ulinzi cha kudumu katika eneo hili, na waweke walinzi wetu wa kudumu hapa badala ya kutegemea kufanya patrol (doria) na kuondoka, kwasababu eneo hili wananchi wanaamini lina madini ya dhahabu kwahivo kila siku wataendelea kuja kujaribu kuvuna dhahabu kutoka hapa.

“Kwasababu sisi kazi yetu ni kuhifadhi Maliasili ambayo tumepata kama urithi wa nchi yetu, niwahakikishie kwamba tutaimarisha ulinzi kwa kuanzisha kituo cha ulinzi hapa ili askari wawe wanabadilishana na kudhibiti kabisa uharibu ambao umekuwa ukifanyika, kwasababu maji yanayotoka katika chanzo hiki yanakwenda kunywesha Muheza yenyewe na wilaya wa Tanga, tukiharibu hapa yatakosekana maji safi na salama”  alisema Dk. Kigwangalla.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala huyo, Prof. Dos Santos Silayo alisema pamoja na eneo hilo kwa sasa kuwa linalindwa na askari wa Suma JKT watahakikisha ulinzi unakuwepo muda wote kwa kutekeleza agizo hilo la Waziri la kujenga kituo cha ulinzi cha kudumu ili askari wawepo katika eneo hilo muda wote.

“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba wananchi hawaingii ili tusiwe tunawashtukiza kuwakamata na kwachukulia hatua, lazima tuwe watu wa kuzuia uhalifu usitokee, nia yetu ni kuwa na kituo mara moja kama alivyoelekeza Mhe. Waziri na hili jambo tumelichukua kama maelekezo na tutalitekeleza kwa nguvu kabisa,” alisema Prof. Dos Santos Silayo.

Awali Dk. Kigwangalla alitembelea kikundi cha wafugaji wa vipepeo katika Tarafa ya Amani ambao waliiomba Serikali ifungulie vibali vya kusafirisha bidhaa hiyo nje ya nchi, aliahidi kuyafanyia kazi maombi yao huku akiwataka kutumia fursa ya ufugaji huo kama bidhaa ya utalii kuwavutia watalii wanaotembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani.

Akiwa mkoani Tanga alitembelea pia Kituo cha Mambo ya Kale cha Mapango ya Amboni na kusema Wizara yake itaboresha kituo hicho pamoja na vituo vingine vya Mambo ya Kale ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini viweze kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa.


Katika ziara hiyo ya siku moja mkoani Tanga alitembelea pia shamba la miti ya Mitiki Longuza, Makumbusho ya Shaban Robert na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
Share:

No comments:

SIKILIZA JAMII FM

Blog Archive

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

HABARI KUU WIKI HII

WAENDESHA BLOG

Contact Form



Recent post