Mkoa
wa Dodoma umefanikiwa kujenga viwanda 892 vingi kati ya hivyo vikiwa ni Vidogo
na vya Kati ambavyo vinachochea ukuaji wa uchumi ikiwa ni sehemu ya
mkakati wa Serikali kutekeleza dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Akizungumza
katika Kipindi maalum cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC) Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt.
Binilith Mahenge amesema kuwa Mkoa huo umejipanga vyema kama Makao
Makuu ya Nchi kuhakikisha kuwa dhana ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda inatekelezwa
na wananchi wote kwa vitendo .
Akifafanua
zaidi Dkt. Mahenge amesema kuwa Dodoma ni mahali salama na kuna maeneo
yakutosha kwa ajili ya uwekezaji hivyo wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi
wanakaribishwa kuja kuwekeza.
“Dodoma
tayari tumeanza kutekeleza miradi inayochochea maendeleo ya uchumi wa viwanda
na tunaamini kuwa Dodoma itakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kiunganishi
cha mikoa yote nchini” Alisisitiza Dkt. Mahenge
Aliongeza
kuwa ni vyema Vijana wanaoishi Mkoani Dodoma wakajiunga katika kwenye
Vikundi ili wapatiwe ujuzi utakaowawezesha kujikwamua kiuchumi ikiwemo
kuanzisha viwanda vidogo na shughuli za uzalishaji kwa ujumla.
Pia
aliwaasa wanaotaka kujenga Mkoani Dodoma kuzingatia Mpango Mji
(Master Plan) kwa kuwa Serikali imeshapanga na
itasimiamia mpango mji uliopo kwa faida
ya wananchi wote.
Akitolea
mfano suala la kumiliki Ardhi Mkoani Dodoma Dkt. Mahenge alisema kuwa ni muhimu
kupitia Manispaa ili kuepuka utapeli na usumbufu unaoweza kujitokeza baadae
ikiwa taratibu hazitafuatwa katika kumiliki Ardhi.
Katika
kuhakikisha kuwa Makao Makuu ya nchi yanakuwa katika mpangilio unaovutia tayari
Serikali imepima viwanja kwa ajili ya kujenga majengo ya Ofisi za Wizara ,
Taasisi na Balozi zote katika eneo maalum utakapojengwa mji wa Serikali.
Kipindi
cha TUNATEKELEZA kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na
kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO ambapo awamu hii inawashirikisha wakuu wa
Mikoa yote, baada ya awamu iliyotangulia kuwahusisha Mawaziri wote
na watendaji wengine wa Serikali.
No comments:
Post a Comment