Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amefanikisha kuchangisha kiasi cha Shillingi Millioni sita na laki tano kutoka kwa Taasisi, Mashirika ya Serikali, watu binafsi na wadau wa maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya watumishi katika Makazi ya kulea wazee na wasiojiweza ya Kiilima yaliyopo Wilayaya Bukoba Vijijini Mkoani Kagera.
Akiongoza harambee hiyo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesisitiza wananchi kujitolea kwa hali na mali katika kufanikisha ujenzi wa nyumba hiyo ambao itasaidia kuwaweka karibu watumishi wa makazi yao katika kuwezesha upatikanaji wa huduma stahiki kwa wazee ikiwemo miundombinu bora, matibabu, chakula, malezi, na haki nyingine wanazostahili.
Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wanawajibu wa kuwashirikisha wananchi kuchangia katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
“Niwaombe wananchi wa Kiilima tuwasaidie kile kidogo cha kwako kiwe fedha au nguvu zako tusaidie ujenzi huu wa nyumba hii ya watumishi ikamilike,” alisema Dkt. Ndugulile.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu amewashukuru wadau kwa michango yao na kuwapongeza wananchi kwa kujitolea nguvu zao na kusisitiza matumizi mazuri ya fedha hizo kwa ajili ya kufanikisha juhudi za kukamilisha jengo la nyumba za watumishi wa makazi ya wazee.
Kwa upande wake Kaimu Mfawidhi wa Makazi hayo Bi. Gladness Luiza ameishukuru Serikali na wadau kwa kuwa wasikivu na kuonesha dhamira ya dhati ya kutatua changamoto inayowakabili na kuahidi kuendelea kuwahudumia wazee kwa moyo wa unyenyekevu katika siku zote za maisha yao.
Washiriki wa Harambee hiyo pia waliahidi kuchangia shilingi Millioni 12, mifuko ya saruji 350, mabati 52, magodoro 20, viti vya miguu mitatu 6, masanduku ya huduma ya kwanza 10, na vifaa vingine muhimu vya kuwahudumiwa wazee vilivyoahidiwa kutolewa na Bohari ya Madawa(MSD). Aidha, wadau waliahidi kuendelea kuchangia ujenzi wa kituo hicho ili kuboresha miundombinu na ustawi wa wazee ambao wamechangia kwa kiasiki kubwa maendeleo ya Taifa.
No comments:
Post a Comment