Naibu Waziri wa
Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ameagiza wamiliki wa kampuni za uchimbaji wa
Madini kote nchini kuwapatia mikataba ya kazi wafanyakazi wote pasina kubagua.
Mhe Biteko ametoa
agizo hilo Leo 23 Februari 2018 wakati alipotembelea eneo la uchimbaji wa makaa
ya mawe katika Kijiji na Kata ya Magamba, Wilayani Mbozi linalomilikiwa na
kampuni ya Magamba Coal Mine.
Alisema amejiridhisha
kuwa wafanyakazi wengi katika migodi mbalimbali nchini ukiwemo wa Magamba
hawana mikataba jambo ambalo linafifihisha uhakika wa ajira zao.
Aidha, Naibu Waziri
huyo wa Madini ametoa siku 14 kuanzia Leo 23 Februari 2018 mpaka 9 Machi 2018
kwa kampuni ya Magamba Coal Mine kuwa wamekamilisha taarifa ya utekelezaji wa
maelekekezo ya ukaguzi wa migodi yaliyotolewa kwao na Ofisi ya Madini kanda
hiyo.
Alisema kuwa endapo
watashindwa kufanya hivyo ni wazi kuwa watakuwa wamekiuka masharti ya leseni
zao na wajibu wao kwa jamii inayowazunguka na hivyo Wizara itawachukulia hatua
bila kuchelewa.
Sambamba na hayo pia
kampuni hiyo imetakiwa kuboresha na kuwa na mahusiano chanya na kijiji cha
Magamba na serikali kwa ujumla ikiwemo kusaidia kuboresha baadhi ya maeneo
ikiwemo sekta ya afya na elimu.
Naibu Waziri wa
Madini akiwa katika ziara ya kikazi katika Mkoa wa Songwe alisema kuwa serikali
imekusudia kurejesha uchumi fungamanishi kwa wananchi hivyo kampuni haziwezi
kuwa na uchumi imara kama zitasalia kuendesha migodi pasina utaratibu wa
kisheria.
No comments:
Post a Comment