Naibu Waziri wa Afya Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amepiga marufuku
dawa za serikali kuonekana zikiuzwa kwenye maduka ya watu binafsi kwani serikali
haitaki kuingia kwenye matatizo ya uhaba wa dawa kwenye sehemu zake za kutolewa
huduma ya afya.
Dk. Ndugulile
amepiga marufuku dawa za serikali kuonekana zikiuzwa kwenye maduka ya watu
binafsi wakati wa ziara yake ya kikazi katika wilaya ya Shinyanga,
Februari 21,2018 akikagua shughuli za huduma za afya zinavyotolewa kwa
wananchi pamoja na kutoa hamasa kwa jamii kujiunga na Bima ya afya ya jamii CHF
iliyoboreshwa.
Dk. Ndugulile alisema katika bajeti
ya mwaka wa fedha (2017-18) serikali kwenye bajeti ya wizara hiyo ya afya
imetenga jumla ya shilingi bilioni 270, tofauti na mwaka wa fedha (2015-16)
ambapo zilikuwa milioni 30 hivyo hawatarajii kusikia sehemu za kutolewa huduma
zake za kiafya kuwa zina upungufu wa dawa.
Akiwa katika hospitali ya Rufaa
ya mkoa wa Shinyanga na Kituo cha Afya cha Kambarage manispaa ya Shinyanga na
kukagua bohari za dawa, Dk. Ndugulile alitoa tahadhari kwa wauguzi kuwa ni
marufuku dawa hizo za serikali kukutwa zinauzwa kwenye maduka ya watu binafsi
na ikibainika watachukuliwa hatua kali.
“Serikali ya awamu hii ya tano
imedhamiria kuboresha huduma za afya hapa nchini, na ndio maana hata bajeti
yake imetolewa ni ya fedha nyingi hivyo sisi kama wizara husika hatutarajii kuwepo
kwa upungufu wa dawa kwenye sehemu za huduma za afya”,alieleza.
Pia aliwataka wananchi kujiunga
na Bima ya afya ya jamii CHF iliyoboreshwa, ili kuwa na uhakika wa kupata
matibabu hasa pale watakapougua na kukutwa hawana pesa ambapo wataweza kutibiwa
kwa shilingi hiyo 10,000/= ili kuokoa maisha yao.
Naye kiongozi wa Mradi wa
Maendeleo ya Tuimarishe Afya (HPSS) kutoka makao makuu Dodoma Profesa Manoris
Meshack, alisema mradi huo wa Bima ya afya ya jamii CHF ulianza mwaka 2011
mkoani Dodoma, na baada ya kufanya vizuri mwaka 2015 ukaongezwa katika mikoa miwili
ya Shinyanga na Morogoro.
Alitaja takwimu za kaya katika
mikoa hiyo mitatu zilizojiunga na CHF iliyoboreshwa hadi sasa kuwa ni 318,334
sawa na asilimia 26 kati ya kaya 1,220,413, na hadi kufikia Disemba 2017
kupitia uandikishaji wa wanachma wamekusanya shilingi bilioni 7,027,605,547.
ambapo shilingi bilioni 2,435,194,000 ni malipo ya tele tele.
Nao baadhi ya wazee kati ya
kumi wasiojiweza ambao walikatiwa Bima hiyo ya Afya ya jamii CHF iliyoboreshwa
na Naibu Waziri huyo wakati wa ziara hiyo,Mohamed Mkumbola na Regina Kulwa
waliipongeza serikali kwa kujali makundi hayo maalumu, na kuomba wazee wote
wakatiwe Bima hiyo pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wajiunge.
No comments:
Post a Comment