Dk. Musagasa akizungumza wakati wa mafunzo hayo. Aliwataka watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kuzingatia matumizi sahihi ya dawa zinazofubaza makali ya VVU pamoja na kuzingatia lishe bora.
Imeelezwa kuwa watu wengi
wanaendelea kupata maambukizi ya Virusi vya #Ukimwi (VVU) kutokana na kuanza
mahusiano ya kimapenzi bila kutambua afya zao hali inayosababisha waanze kuishi
kama mume na mke bila kujua hali zao za kiafya.
Hayo yamesemwa leo
Februari 14,2018 na wahudumu wa jamii wanaosaidia kazi katika vituo vya tiba na
matunzo kwa watu wanaoishi na Maambukizi ya VVU vilivyopo katika halmashauri 7
za wilaya mkoani Mwanza yanayofanyika katika ukumbi wa hotel ya Midland jijini
Mwanza.
Wahudumu hao wapo
katika #mafunzo ya msaada na huduma za kisaikolojia yanayotolewa na Shirika la
Ariel Glaser Pediatric #AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) kwa ufadhili wa Watu
wa Marekani kupitia Centres for Disease Control (CDC).
Wahudumu walisema
kitendo cha kuanza mahusiano ya kimapenzi na kuoana bila kutambua afya ni
miongoni mwa tabia hatarishi zinazochangia kwa kiasi kikubwa kuambukizana VVU.
Mmoja wa washiriki hao
Chausiku Sitta kutoka halmashauri ya wilaya ya Kwimba alieleza kuwa vijana
wanapata maambukizi ya VVU kutokana na kukosa elimu sahihi juu ya VVU na Ukimwi
na wengi wao kutawaliwa na tamaa ya ngono isiyo salama na kudhani kuwa kila mtu
anayeonekana kuwa na umbo zuri basi hana maambukizi ya VVU.
“Vijana wanakurupuka tu,tena
wakiona mwanaume ana mvuto ama mwanamke ana makalio makubwa wao wanaita
‘wowowo’ wanachanganyikiwa kabisa,ndugu zangu huwezi kumtambua mtu mwenye
maambukizi ya VVU kwa kumwangalia kwa macho mpaka apimwe”,aliongeza Chausiku.
Naye Musa Ordas kutoka
halmashauri ya wilaya ya Buchosa aliitaka jamii kutoendekeza waganga wa jadi
kwani baadhi yao wanawadanganya watu wanaoishi na VVU kuwa wamerogwa kwa
kuwalaghai kuwa wametupiwa majini mahaba.
Kwa upande wake,
Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Dk. Joseph Musagasa aliwataka wanaume kuacha
tabia ya kutumia majibu ya wake zao wanapopima VVU kwani majibu yanatofautiana
na hutokea wakati mwingine mmoja kati yao kuwa na maambukizi na mwingine
kutokuwa nayo.
Dk. Musagasa
aliwashauri akina mama #kupima #afya zao kabla ya kubeba ujauzito,na kujifungulia
katika vituo vya afya ili kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto.
“Siyo watoto wote wanaozaliwa
na mama mwenye maambukizi ya VVU wana VVU,hivyo mama unapotaka kubeba mimba
pima kwanza afya yako,ukibainika una maambukizi utashauriwa na wataalamu wa
afya namna ya kufanya ili usimwambukize mtoto wako”,alieleza Dk. Musagasa.
No comments:
Post a Comment