#Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Lushoto (DCC)
imeamua kusitisha mpango wa ujenzi wa #jengo la Halmashauri ya #Bumbuli lilokuwa
lijengwe kwenye eneo jipya la Kwehangala hadi hapo suluhu ya mgogoro baina ya viongozi
wa halmashauri hiyo itakapopatikana.
Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Wilaya
ya Lushoto January Lugangika alisema kuwa maamuzi hayo yamefikiwa baada ya
kuwepo sintofahamu kati ya Madiwani wa halmashauri hiyo na viongozi wengine juu
ya suala hilo. .
Hivi karibuni kumekuwepo na mvutano mkubwa kati ya
viongozi hao juu ya wapi pajengwe majango ya makao makuu ya Halmashauri hiyo. Baadhi ya
viongozi wanadai utaratibu wa fedha za manunuzi haukufuatwa katika
kufikia maamuzi ya kujenga jengo la Halmashauri katika eneo la Kwehangala na
kuacha majengo yaliyokwisha jengwa Bumbuli kwa gharama ya Sh. Milioni 700.
Kutokana na mvutano huo, Mkuu huyo wa Wilaya
amesema kikao kiliafiki kisitishe zoezi hilo mpaka maelewano
yatakapopatikana. ” Wajumbe wameshauri suala la kuhamisha makao makuu lisitishwe
hadi hapo utakapopatikana utangamano, kwani tayari imeonekana kuna mgogoro ambao
umeleta utengano kwa viongozi” Alisema Lugangika . Mbunge wa
jimbo hilo, January Makamba alikiri kuwepo kwa mvutano huo ambao alisema hauna
tija katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Bumbuli.
Makamba alisema ni vyema kama viongozi
wakazungumzia suala la maendeleo mfano;maji,barabara,umeme,nyumba za watumishi
badala ya kila siku kuzungumzia wapi kujengwe jengo la halmashauri. Alishauri
kuwa wananchi washirikishwe katika suala hilo, ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu
ya kutosha juu ya hoja ya kuhamisha halmashauri kwa kuwa ndio wenye chombo chao
badala ya viongozi kuamua wao pekee.
“Suala hilo nakubaliana na maoni wa kikao cha DCC
tulisitishe kwani kwa sasa hatuna shida na majengo ya halmashauri kwa sababu
majengo tunayo ambayo hatulipii kodi ya pango. Sasa hivi tuzungumzie maendeleo
kwani wananchi mwaka 2020 hawatatudai majengo ya halmashauri bali watatudai
maendeleo juu ya huduma muhimu za jamii alisema Makamba. Hivi karibuni
baadhi ya Madiwani wa Halmashauri hiyo walipiga kura ya kupitisha azimio
la kujenga jengo hilo la halmashauri huku Madiwani nane wakigoma kupiga
kura kwa madai kuwa hawawezi kupiga kura wakati kuna ukiukwaji wa kanuni na
utaratibu ktk kitengo cha manunuzi.
Madiwani hao nane ambao waligoma kupiga kura
kupitisha azimio hilo mnamo January 18 mwaka huu walimuomba Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi kuingilia kati mgogoro na kuzuia walichokiita
ukiukwaji wa utaratibu wa manunuzi pamoja na maelekezo mbalimbali ya
viongozi juu ya mpango huo.
Pia walimuomba aingilie kati na kuchukua hatua
dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma na ukiukwaji wa utaratibu wa
uendeshaji wa halmashauri na kudharau kwa makusudi maelekezo yaliyotolewa na
viongozi mbalimbali wa serikali kuu.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Amir Shehiza
alisema kuwa baraza ni chombo chenye maamuzi sahihi hivyo alikitaka Kikao
hicho cha DCC kuacha kuingilia Kazi za baraza.
No comments:
Post a Comment