BENKI
mbalimbali nchini zimewahakikishia wafanyabiashara wa zao la pamba kuwa zina
fedha za kutosha kuweza kuwakopesha ili wanunue pamba yote itakayozalishwa
katika msimu wa mwaka huu nchini.
Pia
viongozi wa benki hizo wamesema wako tayari kusaidia katika uwekezaji wa
miundombinu ya aina yeyote ama eneo litakalohitaji mkopo wa fedha ili
kufanikisha mchakato wa ununuzi wa pamba katika msimu huu ikiwa ni pamoja na
kusaidia ujenzi wa maghala.
Hayo
yamesemwa leo (Jumatano, Februari 21, 2018) na viongozi wa benki mbalimbali
nchini katika mkutano ulioitishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa uliowahusisha
wafanyabiashara wote wa pamba , Wakuu wa Mikoa ,Viongozi wa Halmashauri na
wadau wote.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti viongozi wa benki za NMB, CRDB, TIB, EXIM, AZANIA,
Mkombozi, Bank of Africa, Equity na Eco waliwahakikishia wafanyabiasha hao
mbele ya Waziri Mkuu kwamba wana fedha za kutosha na wako tayari kuwapa mikopo
ili wakanunue pamba mara msimu utakapoanza.
Akizungumza
katika mkutano huo, Waziri Mkuu amewataka wanunuzi wa zao hilo kuandikisha
katika ofisi ya Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba kiasi cha pamba wanachohitaji
kununua pamoja na maeneo ambayo wanatamani kwenda kununua.
Waziri Mkuu amesema suala hilo litaiwezesha bodi kufahamu idadi ya
wafanyabiashara watakaonunua pamba pamoja na kiasi wanachohitaji na eneo
husika. “Serikali itaendelea kusimamia zao hilo kikamilifu.”
Amesema kwa sasa wanauhakika kuwa pamba yote itanunuliwa kwa sababu benki
zimewathibitishia kwamba ziko tayari kuwakopesha wafanyabiasha, hivyo wadau
wote watambue kuwa Serikali itashirikiana nao hadi katika hatua za mwisho za
ununuzi.
Waziri Mkuu aliwahakikishia wafanyabiashara hao kwamba maombi waliyoyatoa
kuhusu uboreshaji wa mauzo ya zao hilo yatayafanyiwa kazi na Serikali
itaendelea kusimamia zao hilo ili ununuzi wake uwe rahisi.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba amesema
wamejipanga kikamilifu katika kudhibiti ubora wa pamba, ambapo amewataka
viongozi wa maghala wasipokee pamba chafu.
Pia amewataka wakulima wa pamba wasithubutu kuchanganya na maji, mawe au
mchanga kwa sababu wataharibu soko. Serikali itapambana na watu wote
wakaothubutu kuharibu zao hilo kwa kcuhukua hatua kali za kisheria kwani huo ni
uhujumu uchumi.
Aliendelea kusema kuwa uamuzi wa Serikali kusimamia ongezeko la
uzalishaji wa zao la pamba unakwenda sambamba na mazao mengine makuu ya
biashara ambayo ni korosho, chai, tumbaku, kahawa na mahindi kwa upande wa chakula.
Dkt. Tizeba amesema inatazamiwa kuwa ifikapo 2021 mchango wa mazao katika
pato la Taifa unakadiriwa kufikia sh. trilioni 13.6, ambapo yataliwezesha Taifa
kuvuka mstari wa kiwango cha umasikini.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa zao la pamba
lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, hivyo watahakikisha zao hilo
linaendelea kukua.
Dkt. Mpango amezitaka benki zichukue tahadhari kwa mikopo chechefu
hivyo wajiridhishe kama wakopaji wote wanatumia mikopo hiyo kwa mujibu wa
makusudio.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 21, 2018.
No comments:
Post a Comment