Mapema mwezi huu, Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya Mtwara imefanya ziara katika Kata ya Nanguruwe yenye lengo la kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Jengo la kupokelea wagonjwa (OPD) katika Kituo cha Afya ambacho kipo katika hatua nzuri ya kupandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Mtwara Vijijini.
Ujenzi huo unaotekelezwa na Mkandarasi Mzalendo Kutoka Jeshi la Kujenga Taifa yaani Kampuni ya Suma JKT unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa robo hii ya pili kulingana na Mkataba, hapo awali kulikuwa na hali ya kusuasua katika utekelezaji hadi pale timu ya wataalamu walipofanya ufuatiliaji wa kina kwa kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani kisha wakaomba wakutane na Mkandarasi ili kujadiliana baadhi ya mambo.
Kabla ya ziara hiyo Kamati ya fedha ilifanya mazungumzo ya kina na Uongozi wa Jeshi hilo katika ukumbi wa Halmashauri kwa lengo la kutathmini maendeleo ya mradi husika na kuainisha changamoto zinazoukabili mradi huo, uongozi wa JKT na Halmashauri ulifikia muafaka wa kuhakikisha kuwa kazi inafanyika kwa Haraka na Usahihi kwakuwa fedha yote ya Mradi ipo.
Kutokana na Mtwara Vijijini kukosa Hospitali yao Viongozi wake wakiongozwa na Mhe. Hawa A. Ghasia (Mb) wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanaisemea kero hiyo kila wapatapo nafasi hali iliyosikika na upande wa Serikali wakaamua kuwa Kituo cha Afya Nanguruwe kifanyiwe upanuzi kwa kujenga majengo mapya, kuboresha yaliyopo kulingana na mahitaji yanayotakiwa katika Hospitali.
Kutokana na hali hiyo kilianza kufanya kazi chache zinazoshabihiana na hospitali ikiwepo kulaza wagonjwa, kufanya upasuaji wa kawaida na Uzazi, kupokea wagonjwa wa sehemu mbalimbali, Ujenzi wa Duka la Dawa la Serikali katika eneo la Kituo na kuongeza Vifaa na Wataalamu wa kutoa huduma za Afya.
Inaaminika kuwa Jengo la Kupokelea wagonjwa linalojengwa likikamilika litakuwa na muonekano wa Kisasa zaidi lenye kupokea wagonjwa wengi sana na kutoa huduma nyingi kwa wakati mmoja, kwa mujibu wa msimamizi wa Ujenzi huo ambaye ni Mhandisi wa Halmashauri Ndg. Frank Kiunga, ameeleza kuwa kwa hali ya sasa mradi unaenda kama ilivyopangwa na inategemewa kasi hii itafanikisha ujenzi kumalizika kwa wakati.
“Kusema ukweli mradi huu kwa sasa unaenda vizuri na kasi ambayo tuliitegemea ingaa hapo awali kulikuwa na kusuasua lakini hii hali ikienda hadi mwisho basi huu mradi utakamailika kwa wakati kabisa kwa kuwa kila kinachohitajika kipo hususani fedha yake yote” alimalizia Mhandisi Kiunga.
Wajumbe wa kamati ya fedha walilidhishwa na hali ya mradi, wamemuagiza Mkurugenzi kuendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu wa mradi huo ili umalizike kwa wakati, pia kamati hiyo ilimtaka Mganga Mkuu wa Wilaya kufanya usimamizi wa karibu wa Zahanati na Vituo vya Afya ili huduma zinazotolewa ziwe muarobaini sahihi wa kutatua kero za afya kwa wananchi.
Juuu ya hapo waliitaka kusimamia kwa umakini matumizi ya fedha yote 750 Milioni iliyoletwa kwaajili ya ujenzi wa Jengo hilo kwasababu kufanikiwa kwake kutaleta matumaini ya kuletewa kiasi kingine cha fedha kwa wakati ilikumalizia Hospitali hiyo na miradi mingine.
chanzo: manispaa
No comments:
Post a Comment