Jeshi la polisi Morogoro limewakamata watu wawili ambao wanadaiwa kuwa ni watekaji wa watu na kujihusisha na matukio ya ubakaji kisha kuwapiga picha za utupu waliowafanyia vitendo hivyo kwa lengo la kuwatisha kusambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP Ulrich Matei amethibitisha kukamatwa kwa watu hao wawili na kusema kuwa wapo watu wengine watatu pia wamekamatwa kwa kufanya wizi kupitia njia ya mitandao ya kijamii.
"Ni kweli tumemkamata mtuhumiwa mmoja akiwa na mwenzake wanaojihusisha na utekaji wa watu, kuwabaka kisha kuwapiga picha za utupu na kuwatishia kuzisambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii kama hawata toa fedha lakini mbali na hao wawili tunawashikilia watu wengine watatu ambao wao wamekuwa wakifanya wizi na utapeli kwa njia za mitandao ya kijamii" alisema Kamanda Matei
Aidha Kamanda Matei amesema kuwa uchunguzi utakapokamilika watu hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao kutokana na makosa hayo.
No comments:
Post a Comment