Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe amewahakikishia
wananchi wa Tanzania kuwa hoja yake aliyoiwakilisha kwa Katibu wa Bunge kuwa
haiwezi kukwamishwa na jambo lolote kwa madai hakuna kisichojulikana
kinachoendelea kutoka katika nchi.
Bashe ametoa kauli hiyo jana (Machi 08, 2018) wakati
alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kwa lengo la
kuelezea sababu zilizompelekea yeye kama Mbunge kuandika barua ya kutaka
kuundwe kwa kamati ya uchunguzi dhidi ya matukio mbalimbali yanayoonesha
kutishia umoja, usalama na mshikamano wa taifa la Tanzania.
"Madhumuni ya kikatiba ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) ni kuwasemea wananchi, kuwatetea kwa hiyo natimiza wajibu
wangu kama Mbunge sioni kama nitapoteza Ubunge wangu katika hili.
"Mimi ninaamini nitapoteza ubunge wangu
kwasababu zifuatazo, endapo nitashindwa kutimiza wajibu wangu ndani ya Bunge,
nikishindwa kutimiza wajibu wangu ndani ya Jimbo langu kwa maana nimeshindwa
kuisimamia serikali katika kuleta maendeleo, nimeshindwa kutimiza ahadi wakati
wa uchaguzi katika jimbo langu na mwisho wanaccm watakaposema kwenye mchakato
wa kidemokrasia wa kura kwamba Hussein wewe hapana.
"Mimi ni muumini wa kiislamu ninaamini kila
binadamu umauti utamfika (kifo) na chochote kitakachonifika ni kile ambacho
amekipanga Mwenyezi Mungu lakini sina hofu yeyote kwasababu hili sio taifa la
namna hiyo.
"Nikiwa kama Hussein sidhani hii hoja kama
inakwenda kukwama kwasababu unapoikwamisha hoja unapaswa kusema unaikwamisha
kwa kutumia misingi gani kama watu wanaamini kwa kila kinachotokea ndani ya
ardhi ya Tanzania sioni kama itakwama.
"Bunge limeshafanya maamuzi mbalimbali juu ya
masuala mbalimbali katika rekodi ya nchi hii, kwa hiyo mimi nadhani ni muhimu
tukatoa fursa jambo hili lifike Bungeni na likifika huko kama litakataliwa basi
tujue ni kwasababu zipi na kama nilivyofanya kuwaambia watanzania ndivyo
hivyo nitarudi kuwaambia limekataliwa kwasababu zipi na hapo tutajadili hatua
za kufanya".
Kwa upande mwingine, Bashe amesema anasubiria majibu
ya barua aliyotuma kutoka kwa Katibu wa Bunge Pamoja na Katibu Chama cha
Mapinduzi (CCM) ambayo ameeleza dhamira na nia yake huku akisisitiza zaidi kuwa
jambo hilo hajalifanya kwa mihemuko (kukurupuka) bali amefanya kwa umakini wa
hali ya juu na utafiti wa kutosha.
No comments:
Post a Comment