DAR ES SALAAM: SERIKALI YAONGEZA HUDUMA ZA MATIBABU YA UGONJWA WA FIGO

SERIKALI kupitia Wizara wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imeongeza wigo wa kutoa huduma za matibabu ya ugonjwa wa figo nchini kwa kuongeza vituo vya usafishaji damu hadi kufikia vituo  zaidi ya 17, na kufanya mafunzo kwa madaktari bingwa ili kuongezea nguvu madaktari bingwa 13 waliopo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile wakati wa matembezi ya Siku ya figo duniani ambayo yamefanyika mapema leo katika viwanja vya Farasi Oysterbay jijini Dar es salaam.
“Wataalamu tunao 13 kwa upande wa madaktari, tumeiona hiyo changamoto kama Serikali, tumeongeza wigo wakufanya mafunzo kwa madaktari bingwa, na hivi karibuni tutatangaza ufadhili kupitia Serikali, vile vile tumetenga fedha kwaajili ya kuwafundisha madaktari ili kuweza kufanya matibabu ya figo” alisema Dkt. Ndugulile.
Dkt. Ndugulile aliendelea kusema kwamba Serikali imeongeza wigo wa usafishaji damu kwa kuongeza vituo Zaidi ya 17 ambavyo vinatoa huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa Figo katika hospitali binafsi na Hospitali za Serikali.
“Tumeongeza wigo wa usafishaji damu hadi tunavyoongea, tunavituo Zaidi ya 17 ambavyo vinatoa huduma ya kusafisha damu katika hospitali binafsi pamoja na hospitali zetu za Serikali , Muhimbili kuna vitanda 42, Mloganzira kuna vitanda 12, Bugando vitanda 6, KCMC vitanda 6, Mbeya vitanda 6, bila kusahau Regency, TMJ, Agakhan, Hindumandal,  na tunaendelea kuimarisha huduma”. Alisema Dkt. Ndugulile.
Vile vile Dkt. Ndugulile alisema kuwa Serikali imeanza upandikizaji wa Figo na imeshafanikisha kwa mgonjwa mmoja mpaka sasa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  na matarajio ni kufanya upasuaji kwa mgonjwa mmoja kila mwezi mmoja.
Aliendelea kusema  mgonjwa mmoja anahitaji wastani wa shilingi milioni 37 kwa mwaka kwa ajili ya kulipia gharama ya kusafisha damu. Aidha, anahitaji kusafiri na kufika kwenye huduma kwa wastani wa safari 126 kwa mwaka sawa na wastani wa safari 3 hadi 4 kwa wiki.
Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile aliendelea kuwa kukumbusha kuwa Serikali ya awamu ya tano imeongeza Bajeti ya Dawa kutoka Bilioni 30 ilipokuwa ikiingia madarakani hadi sasa ni Bilioni 270 kwaajili ya Dawa, vifaa na vifaa tiba kwaajili ya magonjwa yakiwemo magonjwa ya Figo.
“Tumeongeza bajeti kwaajili ya Vifaa, Dawa na Vifaa Tiba kutoka Bilioni 30 wakati Serikali hii inaingia madarakani mbaka Bilioni 270, yaani mara tisa Zaidi, kwahiyo Dawa na Vifaa Tiba kwaajili ya matibabu ya Figo tunazo” alisema Dkt. Ndugulile.
Mwisho Dkt.Ndugulile alitoa wito kwa wananchi kubadili jinsi ya kuandaa vyakula nyumbani, mfano kwa kupunguza kiasi cha chumvi kwenye chakula na kiasi cha mafuta kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza magonjwa shinikizo la damu (hypertension), kisukari na unene wa kupindukia, vile vile kuhamasisha familia kufanya mazoezi.
“Watanzania hatujui kula, tunakula bora chakula kuliko chakula bora, Matumizi ya vyakula vya mafuta, matumizi ya chumvi nyingi, matumizi ya vilevi, matumizi ya sigara kama hayana ulazima basi tupunguze, tutumie vyakula vilivyochemshwa na vilivyochomwa, bila kusahau kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi angalau mara 3 kwa wiki kwa lisaa limoja inatosha” alisema Dkt. Ndugulile.
CHANZO: WIZARA YA AFYA - WAMJW
Share:

No comments:

SIKILIZA JAMII FM

Blog Archive

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

HABARI KUU WIKI HII

WAENDESHA BLOG

Contact Form



Recent post