Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe akionesha namna miundo mbinu ya maji itakavyojengwa kutoka katika mitambo ya maji ya Mailimbili, mjini Dodoma hadi eneo la Ihumwa utakapoojengwa mji wa Serikali
Wizara
ya Maji na Umwagiliaji yaanza kutekeleza Agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli
la kufikisha huduma ya maji katika eneo linalojengwa mji wa Serikali, Ihumwa
Mjini Dodoma kwa kuanza kuchimba visima virefu vyenye uwezo wa kuzalisha mita
za ukubwa 600 kwa siku.
Akizungumza
wakati wa Ziara yakukagua maendeleo yautekelezaji wa Agizo hilo Waziri wa Maji
na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa maji mengine yatachukuliwa
kutoka katika matenki ya Maili mbili ambapo maji yanayozalishwa kutoka katika
chanzo cha Makutopora ni lita milioni 71 wakati mahitaji ni lita milioni
46 kwa siku.
Akifafanua
Mhandisi Kamwele amesema kuwa kutokana na kuwepo kwa ziada ya maji katika
matenki ya Maili mbili mjini humo wataweka mtandao wa mabomba kutoka katika
eneo hilo hadi Ihumwa unakojengwa mji wa Serikali ili kuharakisha shughuli za
ujenzi wa mji huo .
“Kiwango
cha maji kinachosukumwa ni lita milioni 61 tu kati ya milioni 71 tunazozalisha
hali inayopelekea tuwe na maji ya ziada ambayo yatasaidia upatikanaji wa
maji ya uhakika hapa Dodoma ambapo ndio Makao Makuu ya Nchi,” alisisitiza
Mhandisi Kamwelwe.
Aliongeza
kuwa moja ya mikakati ya Wizara yake kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Maji
Taka Dodoma (DUWASA) ni kuongeza visima virefu katika eneo la Mtumba
ambapo visima vingine tayari vimechimbwa tangu mwaka jana ili kukidhi mahitaji
ya maji katika Mji huo ambayo ni takribani lita milioni mbili na laki
sita.
Mhandisi
Kamwelwe amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi kisichozidi
miezi mitatu tangu sasa. Kazi
ya uchimbaji wa visima vingine katika eneo la Mtumba nje kidogo ya Mji wa
Dodoma inatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia leo, ikitekelezwa na Wakala wa
Uchimbaji Visima na Mabwawa (DDCA).
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amesema anaridhishwa
na hatua zinazochukuliwa na Wizara hiyo kupitia DUWASA katika kuhakikisha kuwa
mji wa Dodoma unakuwa na maji ya uhakika yatakayochochea ujenzi wa uchumi wa
viwanda na uwekezaji kwa ujumla.
Mradi
wa Kufikisha maji katika mji wa Serikali ni moja ya Maagizo ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliyoyatoa hivi karibuni kwa
Wizara hiyo, pamoja na Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa miundo mbinu ya umeme
inawekwa katika eneo hilo.
CHANZO: Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma
No comments:
Post a Comment