WATANZANIA CHANGAMKIENI FURSA ZA AJIRA NA UTAFITI WA LUGHA YA KISWAHILI KATIKA SOKO LA AFRIKA MASHARIKI

BWatanzania wametakiwa kuchangamkia fursa za utafiti, fursa za ushirikiano wa kitaalamu na fursa za ajira katika kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ili nafasi zinapotangazwa watanzania wenye sifa wajitokeze kwa wingi kupigania nafasi hizo kufundisha lugha ya Kiswahili katika nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.  

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) pamoja na uzinduzi wa kanzi data ya wataalamu wa Kiswahili jana Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mwakyembe amesema kuwa leo hii kiswahili kimetandawaa na kuenea kote duniani huku kikipewa kipaumbele katika nyanja mbalimbali ikiwemo hapa nchini na hata nchi za nje, kwani nchi mbalimbali zimekua zikionyesha mahitaji ya wataalamu wa lugha ya Kiswahili hivyo kuwataka watanzania kuwa sehemu ya mahitaji hayo.

Aidha Mhe. Mwakyembe ameiambia Bodi mpya ya BAKITA kuwa Wizara inaitarajia bodi hiyo kuwa muhimili wa BAKITA na chachu ya kuirejeshea nchi ukombozi na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania kwa kufanya kazi kisayansi zaidi kuliko kutumia nguvu na rasilimali nyingi bila tija.

“Leo tunazindua rasmi bodi ya BAKITA, naamini kuwa mko tayari kufanya kazi hii kwa juhudi, uteuzi wenu umezingatia sana masharti na weledi kwa mujibu wa sheria ya BAKITA  kwani hakuna hata mmoja wenu aliyeteuliwa kwa kubahatisha” amesema Mhe. Mwakyembe.

Akizungumzia kuhusu kanzi data ya wataalamu wa lugha ya Kiswahili nchini Waziri Mwakyembe amesema kuwa kanzi data hiyo itasaidia kuwapata na kuwajua wataalamu wa Kiswahili tulionao nchini kwa ajili ya mahitaji ya ndani na nje ya nchi lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa watanzania wenye sifa sahihi wanapata nafasi za kazi na kueneza  lugha ya Kiswahili duniani hivyo ni wajibu wa Baraza la Kiswahili la Taifa kuboresha kanzi data hiyo ili ikidhi mahitaji ya soko la ajira la wataalamu wa lugha ya Kiswahili.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Suzan Mlawi amesema kuwa wazo la kuwa na kanzi data ya wataalamu wa lugha ya Kiswahili ni jambo kubwa sana na kwa kuwa kanzi data itatumia njia ya Tehama wananchi watahudumiwa kwa haraka kwa  wepesi na kwa usahihi.

Share:

No comments:

SIKILIZA JAMII FM

Blog Archive

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

HABARI KUU WIKI HII

WAENDESHA BLOG

Contact Form



Recent post