Mtandao wa wanawake na katiba/uchaguzi na uongozi leo umekutana na
wahariri wa habari na waandishi waandamizi kujadiliana masuala mbalimbali juu
ya umuhimu wa kuzingatia misingi na usawa wa kijinsia katika siasa na uongozi
nchini.
Akiwasilisha mada kwa wahariri na wanahabari waandamizi katika
mkutano huo, mtoa mada na mjumbe wa WFT, Dk. Dinah Richard Mmbaga aliwataka
wanahabari kuangalia mfumo mzima wa siasa za vyama vingi na nini
kinachoitenganisha siasa ya Tanzania na nchi nyingine bila kujali tofauti za
itikadi za vyama kwenye masuala yanayohusu utu wa mwanamke, ushiriki wa
mwanamke kuchangia fikra za siasa na uongozi.
Aliwataka kuchambua na kuangalia mambo yapi yatakayounganisha
wanasiasa wote katika kutetea masuala ya kitaifa ikiwa ni pamoja na utu na haki
za mwanamke na pia mfumo wa uongozi utakaowezesha vyama vya siasa kuimarisha
demokrasia shirikishi yenye mrengo wa jinsia ndani ya vyama.
Pia kuchambua mfumo wa uongozi unaowezesha vyama kutatua migogoro
ndani ya vyama vyao bila kutumia vitisho, na hususani vinavyoashiria
kumsababisha mwanamke wa Tanzania asipende kushiriki katika shughuili za siasa
au anaposhiriki ajisikie yuko salama.
Kwa upande wake Mjumbe wa Wanawake na Katiba/uchaguzi na uongozi,
Bi. Laeticia Mukurasi akizungumza katika majadiliano hayo, alisema malengo ni
kujadili kwa pamoja umuhimu wa kuzingatia misingi ya usawa wa jinsia katika
masuala ya siasa na uongozi nchini nchini.
Kujenga makubaliano ya pamoja jinsi waandishi wa habari
watakavyochechemua umuhimu wa kuzingatia misingi ya jinsia kwenye masuala ya
siasa na uongozi katika majukumu yao, na kujengeana uwezo wa masuala ya usawa
wa jinsia na uongozi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment