Malawi Yaonesha Nia Kupata Gesi Kutoka Tanzania



Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amekutana na Ujumbe wa Mawaziri wawili kutoka Malawi na kuzungumza kuhusu uwezekano wa Malawi kupata Gesi Asilia kutoka Tanzania na Uendelezaji wa pamoja wa Bonde la Mto Songwe kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji umeme.

Ujumbe wa Malawi uliongozwa na Waziri wa Maliasili, Nishati na Madini, Aggrey Masi na Waziri wa Viwanda, Biashara na Utalii, Henry Mussa ambao waliambatana na Balozi wa Malawi nchini, Hawa Ndilowe na wataalam kutoka Taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara zao.

Waziri Kalemani alikutana na ujumbe huo Februari 12, 2018 katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam ambapo alielezwa dhumuni la ziara hiyo ya Mawaziri hao wawili kutoka nchini Malawi.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Nishati wa Malawi, Aggrey Masi alisema kuwa Malawi inaupungufu mkubwa wa nishati ya umeme na kwamba jitihada mbalimbali zinafanyika kuhakikisha kiwango cha uzalishaji umeme kinaongezeka.

Alisema umeme unaozalishwa nchini humo kwa sasa ni Megawati 140 pekee huku idadi ya watu ikiwa ni milioni 17 kiasi ambacho alisema kimeshindwa kukidhi mahitaji.

“Sasa hivi tumebaki na megawati 140 peke yake, hali siyo shwari; suluhisho la haraka linahitajika ili kuweka mambo sawa. Imani yetu ni kwa Tanzania kutazama namna ya kusaidia katika hili,” alisema.

Alibainisha kwamba chanzo kikuuu cha uzalishaji wa umeme nchini humo ni maporomoko ya maji na kwamba kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, chanzo hicho kimeshindwa kuzalisha umeme wa kutosha kukidhi mahitaji ya kila siku.

Aliongeza kwamba Serikali ya Malawi imeamua kuwa na vyanzo mbadala vya kuzalishia umeme ikiwemo Gesi Asilia hata hivyo alisema hakuna Gesi Asilia inayozalishwa nchini humo na kwamba matarajio yao ni kupata Gesi Asilia kutoka nchini Tanzania.

“Tumefarijika, tumepokelewa vizuri, lengo la ujio wetu ni kubaini uwezekano wa kupata Gesi Asilia kwa ajili ya kuzalisha umeme,” alisema Masi.

Alisema kwamba baada ya tathmini waliyoifanya wamebaini kwamba chanzo cha haraka kinachoweza kuwasaidia kuvuka kwenye upungufu mkubwa wa umeme uliyoikumba nchi hiyo kwa sasa ni Gesi Asilia kutoka nchini Tanzania.

Aliongeza kuwa tayari mwekezaji amepatikana ambaye atazalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia na kwamba atajenga mitambo yake kwenye eneo la Kalonga mpakani mwa Tanzania na Malawi.

Kwa upande wake Waziri Kalemani alisema suala hilo linaweza kujadiliwa baada ya wataalam wa Tanzania kujiridhisha uwezekano wake.

“Tupo tayari kushirikiana, kinachohitajika hapa ni majadiliano ya kitaalam na wataalam wetu waliopo hapa ili kuelewa mwelekeo,” alisema Waziri Kalemani.

Dkt. Kalemani aliwasisitiza wataalam hao kabla hawajafanya majadiliano wanapaswa kuelewa mambo makuu matatu ambayo wingi wa Gesi Asilia iliyopo kwa sasa, matakwa ya Sera ya Nishati na namna ambavyo Gesi hiyo inaweza kusafirishwa hadi huko Kalonga.

“Je tunayo gesi ya kutosha kugawana ama ni ya kutosha kwa matumizi yetu tu? Je Sera inaruhusu suala hilo? Na kama masuala hayo yanakubalika, Je ni vipi tutaifikisha hiyo Gesi huko mpakani?” alihoji Dkt. Kalemani.

Aliueleza ujumbe huo kuandaa mpango wa ombi lao kimaandishi pamoja na kuandika ombi rasmi na kuwasilisha katika utaratibu maalum wa Kiserikali ili majadiliano yafanyike.

Aidha, suala la Uendelezaji wa pamoja wa Bonde la Mto Songwe, Mawaziri hao kwa pamoja walikubaliana kupitia taarifa ya Tume ya Uendelezaji wa Bonde hilo ambayo inaundwa na nchi hizo mbili ili kubaini hatua za kuchukua kwenye kipengele cha kuzalisha umeme.

Miradi inayotarajiwa kutekelezwa katika bonde hilo ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme kiasi cha Megawati 180 ambazo zitagawanya sawa kwa nchi hizo, kilimo cha umwagiliaji, (hekta 6,200) usambazaji wa maji kwa wananchi, ujenzi wa miundombinu ya jamii (bararabara, shule, na vituo vya afya).

Miradi mingine ni uanzishaji wa viwanda vidogo na vya kati, uvuvi, utalii na uboreshaji wa mazingira, hususan kuimarisha kingo za mto ambao ni mpaka wa Tanzania na Malawi

Share:

No comments:

SIKILIZA JAMII FM

Blog Archive

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

HABARI KUU WIKI HII

WAENDESHA BLOG

Contact Form



Recent post