MADINI YA RUBY KUENDELEA KUWANUFAISHA WANANCHI WA LONGIDO



Serikali imewaahidi wakazi wa Kata ya Mundarara katika Wilaya ya Loliondo kuwa itahakikisha madini ya Ruby ambayo yanapatikana katika eneo hilo yanaendelea kuwanufaisha na siyo kuwadidimiza.
Ahadi hiyo ilitolewa na Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Dotto Biteko baada ya kufanya ziara katika Mgodi unaojishughulisha na uchimbaji wa madini hayo na kisha kuzungumza na wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Nyongo na Biteko waliwataka wananchi wa Mundarara kuondoa hofu kuwa neema ya madini hayo yanayopatikana katika maeneo yao haitawanufaisha tena kutokana na kile wanachodai kuwa sheria mbalimbali zilizowekwa na Serikali zinasababisha kupungua kwa Soko lake.
Akizungumza na wananchi hao, Naibu Waziri Biteko aliwaambia kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini inaandaa mwongozo maalum utakaobainisha utaratibu unaopaswa kutumika katika biashara ya kila aina ya madini hapa nchini ili yaweze kuwanufaisha wananchi na Taifa ipasavyo.
“Nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha rasilimali zote zinazopatikana nchini yakiwemo madini, zinalinufaisha Taifa kwa kiwango kinachostahili. Kwa muda mrefu tumekuwa tukiibiwa sana na watu wengine kunufaishwa na rasilimali zetu wenyewe ilhali sisi tunazidi kuwa maskini. Sasa tumeamua kuwa hatutaki kuibiwa tena,” alisisitiza.
Akifafanua zaidi, Biteko alisema kwamba, mwongozo huo unaoandaliwa na Serikali utasaidia hata wananchi wanaozungukwa na Migodi ya Madini kunufaika zaidi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wananchi hao wa Mundarara kuwa na subira wakati Serikali ikishughulikia hoja zao walizoziwasilisha.
Hata hivyo, alibainisha kuwa Serikali imejipanga kuziba mianya yote ya wizi wa rasilimali madini hivyo alitoa wito kwa wote waliozoea kufanya biashara hiyo kwa udanganyifu kuacha mara moja vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.
“Mnapaswa kufanya biashara iliyo safi. Msiiibie Serikali maana tunahitaji kodi na tozo stahiki kutoka biashara hiyo ili zituwezeshe kuwaletea wananchi maendeleo ikiwemo kujenga barabara, hospitali, shule, huduma za maji safi na nyinginezo.” alisema Biteko.
Awali, akiwasilisha taarifa kwa Naibu Mawaziri kwa niaba ya wananchi wa Mundarara, Diwani wa Kata hiyo, Alais Mushao alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto kadhaa, kubwa ikiwa ni kushuka kwa soko la madini ya Ruby, hali inayosababisha kushuka kwa kipato chao hivyo kurudisha nyuma maendeleo.
“Kutokana na idadi ya wanunuzi wa Ruby kuzidi kupungua siku hadi siku, inasababisha wao kujipangia bei wanayoitaka na hivyo sisi kutonufaika,” alisema Mushao.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali ya uasili wa madini ya Ruby kuwa madogomadogo husababisha kupasuka na kupukuchika. Kufuatia hali hiyo, madini hayo yanapokatwa ili kuyaongezea thamani, yanazidi kupoteza uasili na ubora wake hivyo kushusha zaidi thamani yake.
“Kwa hivyo, tunaiomba Serikali iondoe madini haya katika orodha ya madini yanayotakiwa kukatwa ili turuhusiwe kuyauza kama yalivyo, Soko lake lipande nasi tuendelee kunufaika,” alisema Diwani Mushao.
Wakihitimisha Mkutano huo, Naibu Mawaziri Nyongo na Biteko, walipongeza uhusiano mzuri uliopo kati ya Mwekezaji wa Mgodi na wananchi hao ambao walisema ni wa mfano wa kuigwa.
Ilielezwa kuwa pamoja na kusaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya Kata husika, Mwekezaji huyo amewaruhusu wananchi kuchukua na kuchekecha udongo kutoka Mgodini pasipo kuwalipisha chochote.
chanzo: Veronica Simba, Longido
Share:

No comments:

SIKILIZA JAMII FM

Blog Archive

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

HABARI KUU WIKI HII

WAENDESHA BLOG

Contact Form



Recent post