Zikiwa zimepita siku tatu tangu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
jijini Dar es Salaam iwahukumu kifungo cha mwaka mmoja jela wahamiaji haramu 77
kutoka Ethiopia, wengine 83 wamedakwa mkoani Iringa huku dereva aliyekuwa
akiwasafirisha akifanikiwa kutoroka.
Wahamiaji hao walikamatwa wilayani Kilolo mkoani hapa wakiwa safarini kupelekwa Malawi kisha Afrika Kusini.
Hata hivyo katika harakati za kukamatwa kwao, dereva wa lori
mali ya mkazi wa Tukuyu mkoani Mbeya alitoroka.
Raia hao wa Ethiopia walikamatiwa katika Kijiji cha Mbigili
ambapo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji Mkoa wa Iringa, Hope Kawawa
alisema walikamatwa juzi saa kumi na moja jioni karibu na bomba la mafuta la
Tazama.
Alisema wahamiaji hao walipelekwa kituo cha polisi cha Lugalo na
kwamba, kukamatwa kwao kunatokana na taarifa iliyofikishwa Uhamiaji na
wananchi.
Alisema maofisa wa Uhamiaji kwa kushirikiana na polisi
walipowakamata baadhi yao waliwakuta hali zao ni mbaya kutokana na kukosa
chakula kwa siku tatu na pia kuathiriwa na joto kutokana na bodi la lori
walilokuwa wakisafiria kuwa la bati.
“Wahamiaji hawa walikuwa wanasafiri kwenye lori mali ya mkazi wa
Tukuyu mkoani Mbeya, dereva alikimbia na hajapatikana lakini uchunguzi
unaendelea,” alisema.
Aliongeza kuwa wahamiaji hao watafikishwa mahakamani kesho
kujibu mashtaka yanayowakabili.
“Naomba niwaambie madalali wanaosafirisha hawa wahamiaji kuwa
mkoa wa Iringa si mahala salama kuwapitisha kwa kuwa tuko makini saa 24 na
tukiwabaini hatua kali zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.
Alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapohisi baadhi
ya watu si raia wa Tanzania na wanapowaona watu wasiowatambua. Mtanzania
aliyekamatwa akihusishwa na usafirishaji wa wahamiaji hao, Hassan Mwalusanjo
alisema hana anachofahamu.
Alisema aliomba lifti katika gari hilo kutoka Tukuyu kwenda Dar
es Salaam kununua vifaa vya gari wakati gari hilo lilipokuwa likisafirisha
ndizi. Mwalusajo alisema baada ya kushusha ndizi eneo la Mabibo jijini Dar es
Salaam, dereva aliondoka na aliporeja alipanda kurejea Tukuyu.
Alisema walipofika Ilula alishuka kula ndipo dereva alipoondoka
na gari na aliporejea alimuomba amsaidie kusafisha gari.
“Sielewi chochote nilishangaa kuwekwa chini ya ulinzi baada ya
dereva kuniambia nimsaidie kusafisha gari ambako nilikuta makopo ya maji na
mifuko ya mikate,” alisema akiwa chini ya ulinzi.’’
No comments:
Post a Comment