Wito umetolewa kwa
wananchi wote kuanza kulipa Kodi ya Majengo ya mwaka 2017/18 mapema kwa kuwa
ulipaji wa kodi hiyo umerahisishwa ambapo wanaweza kulipa kwa kutumia
njia ya kielektroniki.
Akizungumza jijini
Dar es Salaam hivi karibuni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Charles Kichere alisema hakuna muda utakao ongezwa ifikapo Juni 30, mwaka huu
na badala yake faini itatozwa kwa kila mmiliki wa jengo atakayechelewa kulipa
kodi hiyo.
“Kama mamlaka hatuoni
sababu ya kuongeza muda wa kulipa Kodi ya Majengo ifikapo tarehe 30 Juni 2018
kwasababu tumewarahisishia wananchi ulipaji wa Kodi hii ambapo wanaweza kupata
ankara ya malipo kwa majengo yaliyosajiliwa kwenye tovuti ya TRA au simu ya
mkononi na kufanya malipo katika tawi lolote la Benki ya NMB au CRDB popote
nchini au kwa njia ya mitandao ya simu ya Mpesa, Tigopesa au Halopesa”, alisema
Kichere.
Kamishna Mkuu Kichere
alisema kuwa, wananchi wafuatilie matangazo ya namna ya kulipa Kodi ya Majengo
kwa njia ya kielektroniki katika mitandao ya kijamii na kwenye vyombo
mbalimbali vya habari au wafike katika ofisi za TRA zilizo karibu na maeneo yao
nchi nzima wapate utaratibu wa kulipa kodi hiyo kielektroniki.
Kichere aliongeza kuwa
Kodi ya Majengo inalipwa kwa mujibu wa Sheria hivyo, ni muhimu wananchi walipe
mapema kodi hiyo ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza mwishoni ikiwa ni
pamoja na msongamano wa watu.
“Natoa wito kwa
wananchi kwamba, wasisubiri mpaka mwisho ndio waanze kupanga foleni kwenye
ofisi za TRA, wanatakiwa kulipa kuanzia sasa hivi katika ofisi zetu na wanaweza
kulipa kwa kutumia njia ya kielektroniki kama nilivyoeleza hapo awali, kinyume
na hapo itatubidi tutoze faini kwa atakayechelewa kulipa kodi hii ya majengo,”
alisisitiza Kichere.
Kodi ya Majengo
hulipwa kuanzia mwezi Julai mosi ya mwaka wa fedha husika hadi Juni 30 ya mwaka
unaofuatia kwa kufuata Sheria, kanuni na taratibu, hivyo, muda huu ni
muafaka kwa wananchi kuanza kulipia kodi ya majengo mpaka ifikapo tarehe 30
Juni, 2018.
No comments:
Post a Comment