Hatima ya mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi
maarufu Sugu anayeshtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais
John Magufuli itajulikana kesho.
Sugu na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,
Emmanuel Masonga wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mbeya ambayo kesho Februari 26,2018 itatoa hukumu.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika Desemba 30,2017 eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge jijini
Mbeya.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite anatarajiwa kutoa hukumu
baada ya upande wa mashtaka na ule wa utetezi kukamilisha ushahidi Februari
9,2018.
Jamhuri iliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja cha
sauti iliyodaiwa kurekodiwa na shahidi wa tano, Inspekta Joram Magova.
Upande wa utetezi uliwasilisha mashahidi sita wakiwamo Sugu na
Masonga waliokana kutamka maneno wanayoshtakiwa kuyatoa.
Washtakiwa walitetewa na mawakili Sabina Yongo, Boniface
Mwabukusi na Hekima Mwasipu kabla ya kujitoa na sasa wanawakilishwa na Peter
Kibatala.
Kwa mara ya kwanza, Sugu na Masonga walifikishwa
mahakamani Januari 16 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph
Pande aliyeeleza upelelezi ulikuwa umekamilika na walikuwa tayari kuendelea na
usikilizaji.
No comments:
Post a Comment