Picha kwa mujibu wa mtandao |
WATU watatu wakiwamo wawili ambao walijinadi kuwa wana mafunzo ya kijeshi, wamefariki dunia mkoani Dodoma katika matukio mawili tofauti ya kusombwa na mafuriko.
Vifo hivyo vimesababishwa na mvua kubwa zilizonyesha usiku wa juzi.
Katika tukio la kwanza lililotokea Nzuguni Manispaa ya Dodoma, Diwani wa Kata ya Nzuguni, Aloyce Luhega, alisema kuwa katika eneo hilo watu wawili waliojinadi kuwa na mafunzo ya kijeshi walisombwa na mafuriko wakati wakitoka katika majukumu yao ya kazi majira ya jioni.
Alisema kuwa wakati wakirudi nyumbani, watu hao walifika katika eneo lenye kivuko ambapo pamejengwa daraja la chini ambalo lilikuwa limejaa maji kutoka na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha juzi jioni.
Alieleza kuwa watu hao ambao bado hawajajulikana majina yao, walipofika katika eneo hilo watu waliwashauri wasivuke hadi maji yatakapopungua, lakini walikaidi na kudai kuwa wanaweza kuvuka.
“Walikwenda hadi katikati wakarudi kama mara tatu hivi, lakini mwisho wake wakasema wao wanaweze kuvuka kwa kuwa walishapitia jeshi, lakini wakati wakielekea kuvuka nguvu ya maji iliwashinda na kuwasomba huku tukiwaangalia,” alisema na kuongeza:
“Hatukuwa na la kufanya, tukawafuatilia, lakini kutokana na giza hatukuweza kuwapata hadi leo hii (jana) asubuhi ndipo tumeweza kuwapata wote wawili.”
Alisema miili ya marehemu polisi wameichukua kwa ajili ya hatua nyingine, ikiwamo waliopotelewa na ndugu zao kuitambua.
“Sasa hivi polisi wanalishughulikia suala hili, sisi kama serikali ya kata tumetoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuitafuta miili hiyo hadi kuipata, hatua nyingine wenzetu wa polisi wataifanyia kazi, nitoe wito kwa wananchi wakati huu wa mvua kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari,” alisema Luhega.
Katika tukio jingine, mkazi mmoja wa Kijiji cha Chibwegele Kata ya Mtera Wilaya Mpwapwa, aliyetambulika kwa jina moja la Martha, amefariki dunia baada ya nyumba yake kumwangukia kutokana na mvua iliyonyesha.
Mvua hiyo pia imesababisha kaya 40 za Kitongoji cha Chungu kukosa mahali pa kuishi, baada ya nyumba zao kusombwa.
Diwani wa kata hiyo, Amoni Kodi, alisema mkazi huyo aliyepoteza maisha alikutwa na mkasa huo akiwa ndani ya nyumba yake.
Alisema baada ya kuangukiwa na nyumba majirani walifanikiwa kwenda kumuokoa, lakini walimkuta amefariki dunia huku akiwa amevunjika miguu.
Diwani huyo alisema waathirika wamehifadhiwa na majirani huku serikali ya kata kwa kushirikiana na kamati ya maafa ya wilaya ikijipanga jinsi ya kuwasaidia.
“Waathirika wote wamepatiwa hifadhi na majirani na kwa upande wa serikali ya kata na wilaya tunajipanga jinsi ya kuzisaidia kaya hizo kama vile chakula, maturubai na mabati hatua ambayo tunaamini itawasaidia, “alisema Kodi .
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alipoulizwa alisema hana taarifa za kutosha juu ya matukio hayo na kuahidi kutoa taarifa rasmi baadaye.
Vifo hivyo ni mwendelezo wa matukio ya majanga ya mvua za mafuriko zinazoendelea katika maeneo kadhaa nchini.
Watu watano wameripotiwa wamepoteza maisha wakiwamo ndugu wawili ndani ya siku tatu katika matukio ya kufa maji katika mvua za mafuriko wilaya za Handeni na Lushoto mkoani Tanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, juzi alithibitisha kutokea kwa vifo vinne vilivyotokana na mafuriko na cha mtu mmoja aliyepigwa na radi.
Bukombe alisema Jumamosi 10 jioni wilayani Lushoto watu wawili ambao ni ndugu, Kassim Yahaya na Awadh Yahaya, wakazi wa Kitongoji cha Mbugui Chini walikufa maji wakivuka mto Lukundo.
Naye Mwamini Ally (46), mkazi wa Kijiji cha Rangwi alikufa kwa kusombwa na maji ya mto Ngurumo.Tukio lingine lilitokea Ijumaa jioni katika Kijiji cha Zavuza Kata ya Kiva wilayani Handeni ambapo Mwanahawa Rajab (60) alikufa kwa kusombwa na maji katika bonde la Bangala na Shaban Juma (30), mkazi wa Kijiji cha Mwamgodi Kata ya Msasa wilayani humo alikufa kwa kupigwa na radi.
No comments:
Post a Comment