ZIKIWA zmebaki siku saba kufikia siku ya upandaji miti duniani, Wilaya ya Ilala imeanza rasmi zoezi ilo ikiwa ni uungwaji wake mkono kwa Makamu wa rais, Samia Suluhu ambaye amekuwa akisisitiza kuwa na Tanzania ya kijani.
Zoezi hilo la upandaji miti kwa manispaa ya Ilala limezinduliwa leo katika kata ya Chanika na Mkuu wa Wilaya hiyo, Sophia Mjema ambaye aliambatana na Diwani wa kata hiyo Ojambi Masaburi.
Akizungumza na umati wa wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo, DC Mjema amesema utunzaji wa mazingira nchini unapaswa kuendana na kasi ya upandaji miti ambayo inasaidia kuleta mvua na kusaidia upatikanaji wa hali safi ya hewa.
DC Mjema amewataka wananchi wa Ilala kutunza mazingira yao kwa kuhamasishana kupanda miti kuanzia ngazi ya familia huku akiwaimiza kuwaripoti Serikali za mtaa wale wote ambao wamekuwa wakiharibu mazingira.
" Wananchi kila mmoja kwa nafasi yenu mnapaswa kutunza mazingira, kuhakikisha mnapanda miti kwa wingi hasa katika maeneo yenu na pia kwenye shule za msingi na sekondari, lengo la zoezi hili ni kujenga mazingira yaliyo bora na salama.
" Tumuunge mkono Rais wetu John Magufuli na Mama Samia ambao wamekuwa wakisisitiza kuwa na Tanzania ya kijani. Lakini kingine kwa wakina mama wenzangu wale mnaofanya biashara ya chakula nafahamu umuhimu wa biashara yenu lakini niwatake sasa mpikie majumbani kisha mbebe chakula hicho na kuja kuuza na siyo kupikia barabarani," amesema Sofia.
Sophia amesema upikaji wa chakula kando ya barabara una athari nyingi za kiafya ikiwemo ugonjwa wa kifua kikuu, huku pia akipiga marufuku utemaji holela wa mate.
Kwa upande wake, diwani wa kata hiyo, Ojambi Masaburi alimshukuru DC Mjema kwa kuja kuzindua zoezi hilo katika kata yake huku akimuahidi kushirikiana na wananchi wake katika kuunga mkono upandaji miti.
" Mheshimiwa DC kwanza nikushukuru sana kwa kuja kwenye kata yetu lakini nikuahidi kuwa sisi tupo kamili kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo ikiwemo suala la mazingira bora, afya na usalama wake," amesema Masaburi
CHANZO: MUUNGWANA
Home »
» DC Mjema azindua zoezi la upandaji miti Ilala
No comments:
Post a Comment