DAR ES SALAAM: WATANZANIA WAHIMIZWA KUJIUNGA NA MTANDAO WA MITAJI

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora amewataka wafanyabiashara nchini kuhamasika kujiunga na mtandao wa mitaji ya ubia ili kuimarisha vitega uchumi vyao na pia kusaidia kuanzisha viwanda hapa nchini.
Profesa Kamuzora alisema hayo wakati akizindua Mtandao wa Mitaji ya Ubia Tanzania – Tanzania Venture Capital Network jijini Dar es salaam jana.
Aidha Katibu Mkuu huyo amesema uzinduzi wa mtandao huo umefanyika wakati mwafaka ambapo serikali ya awamu ya tano ipo katika mikakati ya kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda,
Aliwataka wananchi kuacha uoga katika ushiriki wa kuwawezesha kuwepo kwa mitaji ya kutosha kwa ajili ya uimarishaji wa uwekezaji nchini Tanzania.
Alisema serikali kwa sasa inafanya kila linalowezekana kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji yanakuwa bora, ndio maana wameanzisha mchakato wa kutengeneza sera ya maendeleo ya viwanda hasa katika sekta binafsi.
Alisema ni vyema wenye viwanda na wananchi wengine kushiriki katika mchakato huo ili kufanikisha nia ya kuipeleka Tanzania katika nchi ya viwanda. Alisema kwa kuwa na sera sheria nyingi zitabadilika na hivyo kupunguza urasimu na pia vikwazo vya kuwezesha kazi katika masuala ya viwanda na biashara.
Pia alitaka wamiliki wa Ubia huo kushirikiana na Costech katika kuhakikisha kwamba viwanda vinaanzishwa na kuendelezwa.
Alitaka kuwepo na elimu ya fedha na mitaji ili wananchi waweze kuthubutu na kufanikisha mitaji.
Mapema Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr. Reginald Mengi amewataka wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa uwazi, kwa kuzingatia sheria za nchi, na kuwa tayari kujifunza maarifa mapya kila fursa inapojitokeza.
Akisitikishwa na mahudhurio duni ya wafanyabiashara katika hafla hiyo alisema kutofahamu undani wa  soko la mitaji na fursa zake kunatokana na kutokuwa wazi na kufanya biashara kwa kufuata kanuni.
Akizungumzia kuhusu madai ya kuwapo kwa hali kuwa ngumu nchini Dr. Mengi pia amewataka Watanzania kuichukulia hali hiyo kama fursa ya kubuni biashara itakayowawezesha kupata faida kubwa.
Akiutambulisha Mtandao wa Tanzania Venture Capital kwa wadau, Muasisi wake Bw.  Salum Awadh amesema Mtandao huo ni fursa kwa wawekezaji nchini kujipatia mitaji ya kuanzisha ama kuendeleza biashara zao kwa ubia kwa masharti rahisi.
Alisema kwamba wakati umefika kwa Tanzania kusonga mbele kutumia fursa zilizopo duniani za mitaji na kusema jirani zetu wa Kenya wamesonga mbele katika hilo.
Alisema kwamba kutokana na kutojua umuhimu na ushiriki katika mitaji yenye ubia, wananchi wengi wanakimbilia katika mabenki ya biashara ambako pia wanapambana na vikwazo vingine.
Alisema kwa kuwa na kampuni ya mitaji inayoweza kutafuta pia mtaji inayomilikiwa na wananchi wenyewe kupitia mitaji yao kutawezesha kuwapo na uimara wa viwanda na kuongeza idadi zake kwa kuwa mfumo wa fedha wa mitaji ni tofauti na kwenda benki.
Tanzania kwa sasa ina zaidi ya mabenki 50 ambayo yanajishughulisha na mambo mbalimbali yanayogusa biashara na hifadhi ya kawiada.
Alisema mazingira ya sasa yanahitaji mfumo mwingine wa ziada kusaidia upatikanaji wa mitaji nje ya mabenki na kuzinduliwa kwa mtandao wa ubia wa mitaji kutasaidia kuziba pengo lililopo.
Kwa sasa Tanzania kwa rekodi zilizopo inapata asilimia 17 ya mitaji ya ubia ya dola bilioni 2.4 iliyopo duniani huku Kenya ikiwa na nfasi nzuri zaidi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya sekta Binafsi nchini-TPSF Bw. Godfrey Simbeye, baadhi ya viongozi wa taasisi za serikali na wafanyabiashara mbalimbali.
Share:

No comments:

SIKILIZA JAMII FM

Blog Archive

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

HABARI KUU WIKI HII

WAENDESHA BLOG

Contact Form



Recent post