UGANDA: Makubaliano waliyoyafikia wakuu wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki

Mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umemalizika jioni  tarehe 23 Februari, 2018 katika hoteli ya Munyonyo mjini Kampala nchini Uganda.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amehudhuria mkutano huo pamoja na Marais wengine Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta wa Kenya, Mhe. Salva Kiir Mayardit wa Sudani Kusini na Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza amewakilishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Gaston Sindimwo na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame amewakilishwa na Waziri wa Miundombinu Mhe. James Musoni.

Mkutano huo umeongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Yoweri Kaguta Museveni na kwa pamoja Waheshimiwa Marais wamemteua Mhe. Jaji Charles Ayako Nyachae kuwa Jaji wa Mahakama ya Awali ya Afrika Mashariki na Mhe. Jaji Faustin Ntezilyayo kuwa Naibu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Afrika Mashariki kuanzia tarehe 01 Julai, 2018.

Pia wameamua Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na Naibu Makatibu Wakuu wawili badala ya mapendekezo ya kuwa na Naibu Makatibu Wakuu watano.

Aidha, wakuu wa nchi wamezindua mkakati wa tano wa maendeleo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaoanzia 2016/17 hadi 2020/21, wameamua kuendelea na majadiliano kuhusu mkataba wa ubia wa kibiashara kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya (EPA) na wamepokea ripoti ya maendeleo ya majadiliano ya kutafuta amani ya mgogoro wa Burundi kutoka kwa Mratibu wa mazungumzo hayo Mhe. Rais Mstaafu Benjamin Willian Mkapa.

Halikadhalika wakuu wa nchi wamewahimiza wahusika wote katika mgogoro wa Burundi kushirikiana na Mratibu na Msuluhishi wa mgogoro huo ili kufanikisha mazungumzo hayo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kampala
23 Februari, 2018
Share:

No comments:

SIKILIZA JAMII FM

Blog Archive

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

HABARI KUU WIKI HII

WAENDESHA BLOG

Contact Form



Recent post