Upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu na wenzake jana ulidai mahakamani kuwa umefunga ushahidi dhidi ya mashtaka kutumia na kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi kwa msanii huyo.
Madai hayo yalitolewa jana na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakati wa kusikiliza ushahidi wa shahidi wa nne na wa tano mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Awali, shahidi wa nne, mjumbe wa nyumba 10, Steven Ndonde alidai mahakamani hapo kuwa siku ya tukio aliitwa kushuhudia upekuzi nyumbani kwa Sepetu.
Alidai kuwa wakati upekuzi unaendelea walikuta kipisi cha msokoto katika chumba cha nguo na viatu cha msanii huyo na chumba cha mfanyakazi wake walikuta kipisi kingine.
Hata hivyo, shahidi huyo alipohojiwa na wakili wa utetezi Albart Msando alikana kuwakuta washtakiwa wote wakiwa na dawa za kulevya aina ya bangi katika upekuzi huo.
Shahidi wa tano, Koplo wa Polisi Robert (31), alidai kuwa Februari 4, 2017 alipokea maagizo kutoka kwa bosi wake ya kupeleka vielelezo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ikiwamo msokoto mmoja na vipisi viwili vya dawa za kulevya idhaniwayo kuwa bangi.
"Nilipeleka, vilipokelewa ofisi ya mkemia mkuu, baada ya kupokelewa niliandika barua kuhusu vielelezo hivyo," alidai Koplo Robert.
Kakula alidai baada ya kuita mashahidi watato dhidi ya washtakiwa upande wa Jamhuri imefunga kesi yao.
"Mheshimiwa hakimu tunaiachia mahakama iamue sisi upande wa Jamhuri tumefunga kesi yetu..." Alidai Kakula.
Wakili Msando aliomba upande wa utetezi kuwasilisha hoja za kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la ndani ya siku 10.
Upande wa Jamhuri ulidai utawasilisha majibu Aprili 3, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.
Mbali na Sepetu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Angelina Msigwa na Matrida Abbas.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.
Inadaiwa kuwa Februari 4, mwaka jana katika makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio, washtakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.
Ilidaiwa kuwa Februari mosi, mwaka jana katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, Sepetu alitumia dawa za kulevya aina ya bangi. Washtakiwa walikana mashitaka.
No comments:
Post a Comment