Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC) mapema leo limewataka wananchi kupuuza taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba kiwanda cha saruji cha Dangote mkoani Mtwara kimefungwa.
Taarifa kutoka kitengo cha mawasiliano cha shirika hilo imesema taarifa hiyo inayoendelea kusambazwa ni ya mwaka 2016 hivyo imeshapitwa na wakati kwani kiwanda hicho kinaendelea na zoezi la usimikaji wa mitambo yake ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia na kazi hiyo inatarajiqa kumalizika mwezi ujao april mwaka huu.
Aidha,taarifa hiyo imesema Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini(TPDC) tayari lilishatimiza makubaliano yote ikiwemo mauzo ya gesi asilia pamoja na ujenzi wa mitambo ya kusafirishia gesi asilia hadi kwenye mitambo ya kuzalisha umeme ya kiwanda hicho tangu mwaka jana 2017.
Kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara mwaka 2016 kimewahi kuripotiwa kuingia mgogoro na TPDC kwa Kile kilichoelezwa kushindwa kukubaliana na shirika hilo juu ya mauzo ya gesi asilia na kupigwa marufuku kwa kiwanda hicho kutoingiza makaa ya mawe kutoka Afrika Kusini na kutakiwa kutumia ya Liganga ambayo kilidai yapo chini ya kiwango na bei ghali.
No comments:
Post a Comment