Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imemuhukumu Miezi Mitano jela Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite ambapo amesema ameridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mteite amesema kuwa Mahakama imejikita katika sehemu kuu nne.
Amesema kuwa sehemu hizo ni kama washtakiwa walitamka Maneno ya fedheha, pia kama maneno waliyoyatoa yamebeba maudhui ya fedheha, pia kama maneno hayo yana mlenga Rais pamoja washtakiwa kama wana hatia ama lah.
Katika hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa moja Hakimu Mteite amesema amejiridhisha pasina kuacha shaka juu ya ushahidi wa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka.
Hakimu Mteite amesema Mahakama inakubaliana na hoja ya kwamba washtakiwa walitamka maneno ya fedheha dhidi ya Rais kutokana na ushahidi wa upande wa mashtaka ambao waliwasikia washtakiwa na kuwaona wakati wakitamka.
“Katika kesi hii mashahidi wengi ni askari, hivyo ni dhahiri wametoa maneno hayo,” -Hakimu Mteite
Pia kuhusu maneno hayo kumlenga Rais Magufuli, Hakimu Mteite amesema maneno hayo ya fedheha ni ya kitaifa, kwani masuala yanayogusa watu kuuawa ni ya kitaifa na ndio maana washtakiwa walitamka maneno (Rais Wetu).
“Tujiulize ni Rais yupi waliyemzungumzia ni wa Simba, Yanga ama Mbeya City hivyo Rais aliyezungumziwa hapa ni Magufuli kwani hakuna Magufuli mwingine anayetuongoza,”-Hakimu Mteite
Hakimu Mteite amesema kwa imani yake washtakiwa wana hatia.
“Kutokana na upande wa utetezi kuomba nafuu ya adhabu na upande wa mashtaka kutaka itolewe adhabu kali, nawahukumu miezi mitano jela,” -Hakimu Mteite.
CHANZO: MPEKUZI
Home »
» MBEYA: Mbunge Joseph Mbilinyi 'sugu' Kahukumiwa Miezi Mitano Jela
No comments:
Post a Comment