Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo amepata ajali baada ya gari lake kupasuka tairi na kupinduka
Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembo amesema ajali hiyo ilitokea kati ya eneo la Mdori na Minjingu wilayani Babati jana Februari 26 saa nane mchana.
Amesema Kamanda Mkumbo ambaye alikuwa anatoka mkoani Singida kurejea Arusha, ameumia kidole cha mkono wa kushoto na michubuko iliyotokana na kukatwa na vioo.
Amesema gari lilipata ajali baada ya kupasuka tairi la nyuma upande wa kushoto.
Ilembo amesema Mkumbo baada ya kufikishwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, aliingizwa chumba cha upasuaji moja kwa moja.
Pia, katika ajali hiyo dereva wa kamanda Mkumbo, Staff Sajent Silvanus aliumia maeneo ya paja.
Mganga mfawidhi wa Mkoa Arusha, Dk Omar Chande amesema majeruhi wote wanapatiwa matibabu.
Hata hivyo, hakuwa tayari kuelezea hali za majeruhi hasa kwa maelezo kuwa uchunguzi wa kutabibu unaendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa pia wamefika hospitali ya mkoa kumjulia hali Mkumbo na majeruhi wengine.
CHANZO: MPEKUZI
No comments:
Post a Comment