Na Mwandishi Wetu, Kenya.
Anthony Karanja mwenye umri wa miaka 25 anashikiliwa na jeshi la polisi kwa kumuua mkewe kwa kumkata na shoka na kumchoma visu kufuatia ugomvi uliozuka baada ya kupokea ujumbe wa mapenzi kwenye simu yake (ya Karanja).
Kwa mujibu wa Polisi wa eneo la Trans Nzoia nchini Kenya, Karanja alipokea ujumbe huo kwenye simu yake ambao mkewe aliouna na kuanzisha ugomvi kutokana na wivu wa mapenzi, lakini alijibiwa kwa kushambuliwa kwa visu na kumkata na shoka.
Polisi wameeleza kuwa mtuhumiwa ambaye alijisalimisha mwenyewe polisi baada ya kutekeleza mauaji hayo alieleza kuwa alimchoma mkewe Esther Wangui kisu kwenye paja, kwenye miguu na kifuani.
Imeelezwa kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo Jumapili iliyopita, alijaribu kujiua bila mafanikio na ndipo alipofika katika kituo cha polisi akipiga kelele, “Nimemmaliza endeni mumchukue.”
Majirani wameeleza kuwa walisikia ugomvi kati ya wawili hao majira ya saa moja na nusu asubuhi. Wameeleza kuwa baada ya kutekeleza mauaji, mtuhumiwa alikunywa sumu ili ajiue lakini hakufanikiwa ndipo alipoamua kujinyonga kwa kamba lakini pia hakufanikiwa.
“Mtuhumiwa aliwapeleka maafisa wetu nyumbani kwake na akawapa funguo kuwawezesha kuuchukua mwili wa marehemu,” Mkuu wa Polisi wa eneo hilo, Jackson Mwenga anakaririwa.
Mwenga alisema kuwa wanaendelea kumshikilia mtuhumiwa na wameanza kufanya upelelezi.
No comments:
Post a Comment